Na Mwandishi Wetu
Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Temeke, umepokea taarifa za madiwani wa viti maalumu kuhusu utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kipindi cha miezi sita iliyopita na kuahidi kuendelea kuwasimamia kikamilifu madiwani hao kutimiza wajibu wao.
Akizungumza wakati wa Baraza la UWT Temeke, Mwenyekiti wa umoja huo wilayani humo, Lawama Mikidafi, amesema baraza litaendelea kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya CCM na miradi inayotekelezwa wilayani humo.
“Sisi UWT tumejipanga vizuri kuhakikisha kila shughuli inayofanywa na madiwani hawa tunaipata kupitia utekelezaji. Sisi tutazifanyia tathimini na tunamipangokazi tuliyoweka ambayo tunataka ifikiwe,”amesema Lawama.
Akifungua mkutano wa Baraza, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Abass Mtemvu, ameitaka UWT kuimarisha umoja na kuondoa tofauti zao katika kutumikia wananchi ambao wanamatumaini makubwa na Chama.
“Pendaneni na muwe wamoja yaani mtafanya kazi kubwa Temeke. Temeke mnauwezo mkubwa na mnarasilimali nyingi lakini mnashindwa kusaidia kina mama,”amesema Mtemvu.
Mtemvu amesema hata mikopo inayotolewa na halmashauri kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wanaonufaika nayo siyo wanawake CCM.
“Kwa sababu hamuelewani. Hebu wapeni uwezo wanawake hawa kwa sababu siasa ni uchumi. Wafanyeni kina mama wawe na uwezo mtafika mbali,”ameeleza Mtemvu.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa (NEC) ya CCM, Juma Simba ‘Gadaffi’, amesema kutokana na hali inayoendelea ndani ya UWT Temeke lazima kuna sababu zilizo jificha.
“ Tutakaa na UWT, Kamati ya Utekelezaji ya Wilaya. Hapa kuna jambo na hilo jambo inawezekana nongwa za uchaguzi hazijaisha ndani ya UWT, ndani ya Chama wilaya au mkoa,”amesema Simba.
Baadhi ya madiwani wa viti maalumu wilayani humo wamempongeza Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. Samia kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo wilayani humo na kwamba wamejipanga kikamilifu kuhakikisha Chama kinaibuka na ushindi mkubwa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mapema mwakani na Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.