BODI YA MAJI YA TAIFA YATEMBELEA DUWASA KUJIONEA HALI YA MAJI



Bodi ya Maji ya Taifa wametembelea Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) na kufanya kikao kazi na bodi na menejimenti ya Mamlaka hiyo kwa lengo la kujionea hali ya maji kwa jiji la Dodoma.

Akizungumza katika ziara hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya Maji ya Taifa, Mhandisi Mbogo Mfutakamba, amesema maendeleo ya uchumi wa dunia yanategemea na upatikanaji maji ya uhakika hivyo uwekezaji mkubwa unahitajika kuhakikisha vyanzo vya maji vinalindwa.

"Zamani suala la utunzaji vyanzo vya maji lilikuwa jambo gumu kueleweka lakini sasa suala hilo limeanza kutiliwa mkazo," amebainisha.

Mhandisi Mbogo ameeleza kuwa serikali imeipa nguvu bodi hiyo kuhakikisha maji yanaendelea kuwepo kama nyenzo muhimu ya maendeleo ya Taifa.

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya DUWASA, Balozi Job Masima, Mjumbe wa bodi hiyo, Peter Mavunde, amesema DUWASA itaendelea kuhakikisha wakazi wa Dodoma wanaendelea kupata huduma ya maji.

Amewataka wataalamu wa Mamlaka hiyo kuendelea kutumia ujuzi wao kusadia wananchi waendelee kupata huduma hiyo muhimu kwa maendeleo ya nchi.

Amesisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya Mamlaka ya Bonde la Wami/Ruvu na DUWASA katika kutatua changamoto mbalimbali pindi zinapojitokeza.

Naye, Mjumbe wa Bodi ya DUWASA, Profesa Davis Mwamfupe amesema watumiaji wa maji wanapaswa kuwa wa kwanza katika utunzaji vyanzo vya maji.

"Wananchi wafahamu kwamba wao ndio wa kwanza kujiuliza jitihada walizozifanya katika kutunza vyanzo vya maji pindi yanapoadimika na sio kuanza kulaumu Mamlaka za maji," alieleza Profesa Mwafupe ambaye pia ni Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma.

Wakati akiwasilisha taarifa ya utendajikazi wa Mamlaka hiyo kwa ujumbe wa Bodi ya Taifa ya Maji, Mkurugenzi wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph, ameeleza namna usomaji mita shirikishi ulivyosaidia kupunguza kiwango cha upotevu maji.

Amesema usomaji huo umewezesha kubaini uhalisia wa kiwango cha maji alichotumia mtumiaji na kiwango cha ankara ya maji alichotozwa mteja wa Mamlaka hiyo.

"Ushirikishwaji wananchi wakati wa usomaji mita umesaidia sana kupunguza kiwango cha upotevu wa maji kwani tunaweza kufahamu kiwango halisi ambacho mtumiaji ametumia na ankara aliyotozwa.

"Kupitia utaratibu huo, mtumiaji anatumiwa ujumbe mfupi unaoeleza kiwango cha maji alichotumia na kama atakuwa na tatizo anaweza kuwasiliana na Mamlaka kabla ya kiwango hicho kuchakatwa." Amesema Mhandisi Aron.

Amesema DUWASA pia inatumia mfumo wa upigaji picha mita ya mteja kisha kutumwa kwa kwenye mfumo kuhakiki kama mita husika imesomwa kwa usahihi.

Mhandisi Joseph amesema kuwa Mamlaka hiyo inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali yenye lengo la kuongeza kiwango cha upatikanaji maji kwa wakazi wa Jiji la Dodoma.

Hata hivyo, amesema katika mabonde tisa ya maji yaliyopo nchini, maji yanayozungumziwa ni yale ambayo yanaonekana juu ya ardhi na sio yaliyopo chini ya ardhi ambayo ni tegemeo kubwa kwa Mkoa wa Dodoma.

"Changamoto iliyopo maeneo ambayo yenye maji chini ya ardhi hayajatangazwa kama maeneo tengefu na ndio maana ukitaka kwenda kuchimba utakuta tayari yana wamiliki," amesema.

Amebainisha kuwa maji chini ya ardhi ni fursa muhimu lakini inakuwa ngumu kuyafikia kwa sababu maeneo husika yanamilikiwa, hivyo kuongeza gharama kuyafikia.