WANANCHI WAMEASWA KUJIEPUSHA NA VITENDO VYA UKATILI



Na HEMEDI MUNGA

Waumini wa dini mbalimbali wilayani Iramba mkoani Singida wameaswa kujiepusha na vitendo vya kikatili kwa sababu kufanya hivyo ni kujiwekea kumbukumbu mbaya mbele ya Mwenyezi Mungu.

Nasaha hizo zimetolewa na Mkuu wa wilaya hiyo, Suleiman Mwenda, katika msikiti wa Taqwa baada ya swala ya Ijumaa, msikitini hapo.

Amesema waumini wafuate mafundisho ya mema ya Mtume Mohamad (SAW) na amewakumbusha waumini hao na  wananchi wote wilayani hapa kujiepusha na vitendo vya kikatili ambavyo vinadaiwa kuwapo katika maeneo tofauti.m

Mwenda amesema matendo yote wanayoyatenda duniani hata kama itakuwa ni usiku wa manane wenye giza zito na kukimbia kwa lengo la serikali isiwaone  na kuwakamata wakumbuke tukio hilo tayari litakuwa limepata hesabu yake mbele ya Mwenyezi  Mungu.

Amesisitiza kuwa yoyote yale wanayoyafanya wanadamu yakiwa mema au mabaya watayakuta.

" Ndugu zangu fahamuni kuwa serikali inamacho na inaona wanaodaiwa kufanya vitendo vya kikatili tutawakamata," amesema.

Aidha, ameongeza ikiwa hawatokamatwa basi wafahamu kuwa watakutana na Mwenyezi Mungu ambaye ni mkali wa kuadhibu.