WANACHAMA YANGA WATOA ZAWADI KWA WANAFUNZI WENYE MAHITAJI MAALUMU WILAYANI IRAMBA



 

Na Hemed Munga

Wanachama na wapenzi wa klabu ya Yanga wilayani Iramba, wametakiwa kutembea kifua mbele wakiamini msimu huu watachukua tena ubingwa wa Ligi  Kuu ya NBC na FA.

Wito huo umetolewa na Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCMM) Wilaya ya Iramba, Mkoa wa Singida, Amani Daudi, baada ya kutoa zawadi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika Shule ya Msingi Kizega, ambapo amesema klabu yao imesajili vizuri.

Amesema kinachofanyika ni kuonyesha wananchi wameamua kuonesha uwananchi wao kwa vitendo kwa kushiriki pamoja na wanafunzi hao kwa kutoa zawadi mbalimbali.

"Ninawapongeza ndugu zangu kwa kufurahi na watoto ambao ndio wajenzi wa Taifa hili," amesema.

Aidha, amewahakikishia wananchi na wapenzi wa timu hiyo, kuwa mwaka huu watabeba makombe yote ambayo klabu hiyo inashiriki.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kiomboi, wilayani humo, mwanachama wa timu hiyo, Omary Hassan, amesema kwa kuzingatia haki za binadamu, wanadamu wote ni sawa, hivyo wameamua kuwatembelea na kufurahi na wanafunzi hao.

Amesema wenye mamlaka na nchi hii ni wananchi, hivyo ni lazima kwao kuyafikia makundi mbalimbali kwa kutoa zawadi ikiwemo kuwasalimia watoto wao.

"Sisi wananchi tunapokuja kuwatembelea ni sehemu ya kumbukizi ya ukombozi wa  nchi yetu," amesema.

Naye Katibu wa tawi la klabu hiyo namba 3003 mjini Kiomboi,  wilayani humo, Farijala Mumwi, amesema wanatambua wanafunzi hao ni sehemu ya jamii yao, hivyo hawana  budi kutoa zawadi mbalimbali.

Amesema wametoa vitu mbalimbali wakiamini kuwa wanafunzi hao watakuwa na furaha kama waliyonayo wao katika kusherehekea mafanikio ambayo timu ya Yanga iliyapata msimu uliyopita.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Hainess Kiwelu, amewashukuru wanachama wa timu hiyo kwa kuwa na moyo wa upendo kushiriki pamoja na wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

"Sisi tumo ndani yenu na tunamuomba Mungu awabariki sana na kuwapa badala ya kile mlichokitoa," ameomba.

Katibu wa UVCCM wa Wilaya ya Iramba, Mkoa wa Singida, mwanachama wa Klabu ya Yanga, Amani Daudi, akizungumza wakati wa kutoa zawadi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu wa Shule ya Msingi Kizega. (Picha na Hemedi Munga).

Diwani wa Kata ya Kiomboi, wilayani Iramba Mkoa wa Singida, ambaye ni  mwanachama wa Klabu  ya Yanga, Omary Hassan, akizungumza kuhusu mafanikio ya klabu hiyo na kuwahakikishia watachukua makombe yote, baada ya kutoa zawadi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu Shule ya Msingi Kizega.

Wanachama wa Klabu ya Yanga wakiwa na wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika Shule ya Msingi Kizega wilayani Iramba, Mkoa wa Singida. (Picha na Hemedi Munga).