WANAKIJIJI WA MSEKO WALIOGUSWA NA MARADI WA BOMBA LA MAFUTA KUTOKA UGANDA KWENDA TANGA WAKABIDHIWA NYUMBA ZAO

Mkuu wa Wilaya ya Iramba, mkoani Singida, Suleiman Mwenda (kushoto), akizindua nyumba  zilizojengwa na Mpango wa Fidia wa Bomba la Mafuta, kabla ya kuwakabidhi wanakijiji cha Mseko, wilayani humo. (Picha na Hemedi Munga).

Na Hamed Munga

Wananchi walioguswa na mradi wa Bomba la Mafuta kutoka Uganda kwenda Tanga, katika Kijiji cha Mseko wilayani, Iramba, Mkoa wa Singida wamekabidhiwa nyumba zao, pia wametakiwa kufuga kisasa kujiletea maendeleo.

Mkuu wa wilaya hiyo, Suleiman, ametoa wito huo wakati wa kuwakabidhi nyumba wananchi hao, ambapo amewataka kujinufaisha kutokana na mifugo wanayofuga kwa lengo la kupata makazi bora mfano wa nyumba ambazo amewakabizi baadhi yao.

"Ndugu zangu ninaelewa eneo hili ni la wafugaji, hivyo niwaombe tufuge kisasa tena kwa tija," amesisitiza.

Aidha, ameongeza kuwa mwenye ng'ombe zaidi ya 800 au 200 kwa nini asijenge nyumba bora mfano wa hizo alizokabidhi.

Hata hivyo, Mwenda amewataka wananchi hao kuhakikisha wanapanda miti katika maeneo hayo kwa lengo la kutunza mazingira vizuri.

Amesema wananchi walipewa ruhusa yakuamua kupewa fedha au kujengewa nyumba.

"Hakika ninashukuru wananchi wangu wengi walichagua kujengewa nyumba na leo ninawakabidhi, hongereni sana", amesema.

Pia, amesema wamepata nyumba zilizokuwa bora na za kisasa kwa sababu zinamiundombinu iliyokamilika ukilinganisha na thamani ya nyumba zilizokuwepo.

Aidha, amefafanua kuwa nyumba hizo zimejengwa kwa ukuta wa zege, hivyo kuweza kuishi miaka 100.

"Kwa kweli ni nyumba ambazo zinahadhi ya mjini kwa sababu kuna umeme, mfumo wa maji ya mvua, jiko la kisasa na choo Chenye  bafu, hongereni sana," amesema.

Kutokana na kukabidhiwa nyumba hizo kwa walengwa, Mwenda amemuagiza Idara ya Ardhi kwa kushirikiana na Mratibu wa Mpango wa Fidia wa Mradi huo kuhakikisha walengwa wanapata hati miliki za nyumba hizo kwa sababu zitawaongezea thamani na kupata mikopo yakilimo.

Katika hatua nyingine, Mwenda amemuagiza mratibu huyo,  Kasian Ninga kuhakikisha katika maeneo mengine wanayotekeleza ujenzi wa nyumba hizo kuharakisha kwa  lengo la kuhakikisha wananchi wanapata fidia zao kwa wakati.

Aidha, amewapongeza kwa kufanya kazi nzuri za ujenzi wa nyumba hizo.

Kwa upande wa Mratibu wa Mpango wa Fidia wa Mradi huo, Kasian Ninga amesema kuna waguswa 12 ambapo  10 walichagua kujengewa nyumba na wawili ndio walichaguwa kupewa fedha.

Amesema kuwa mpango huo utatoa huduma za kuwahamisha kutoka  walikokuwa wanaishi kabla ya kupanta nyumba hizi, huduma ya chakula kwa wanaostahiki kupata huduma hiyo na huduma za kujikimu kimaisha ikiwemo kupewa elimu ya kilimo na ujasiriliamali.

"Mhe. MKuu wa wilaya utaratibu na sheria zilizotumika  ni kwa kuzingatia viwango vya kimataifa katika miradi mikubwa kama hii," amesema.

Naye mguswa katika mradi huo, Mahola Luhaga ameishukuru serikali kwa kuwatendea haki kwa kukabidiwa nyumba na mkuu huyo wa wilaya.

Mkuu wa Wilaya ya Iramba, mkoani Singida, Suleiman Mwenda, akikagua  nyumba zilizojengwa na Mpango wa Fidia wa Bomba la Mafuta ambapo wanufaika wamekabidhiwa, katika kijiji cha Mseko wilayani humo.  (Picha na Hemedi Munga).