Na HEMEDI MUNGA
Wanafunzi wa Shule za Sekondari wilayani Iramba, mkoani Singida, wametakiwa kuendeleza vipaji vyao kwa lengo la kuhakikisha wanatimiza ndoto zao katika maisha.
Aidha, wametakiwa kuutumia muda na fursa walizozipata katika kipindi ambacho wao ni wanafunzi kwa manufaa ya baadae.
Akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Lulumba, mjini Kiomboi, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Innocent Msengi, amesema hakika kila kiongozi akitembelea shule hiyo anaona kuna vipaji vya kutosha.
Pia, amewapongeza walimu kwa kazi nzuri wanayoifanya, hivyo kuwafanya viongozi wa wilaya hiyo kutembea kifua mbele.
"Niwaombe ndugu zangu watumishi tuendelee na moyo huo wa kufanya kazi kama timu inayoleta matokeo mazuri," amesema.
Kufanya hivyo kunaendelea kuijenga Iramba kitaaluma na kwa kweli viongozi wao wanapenda kuona mafanikio ya kitaaluma.
"Niwaombe wanafunzi wetu hakika vipaji mnavyo vitumieni na muendelee kutulia kwa kujenga maisha yenu ya baadae," amesisitiza.
Amewataka wanafunzi hao kutumia nafasi na fursa kwa kujijengea mipango mizuri itakayowafanya kuwa na nembo katika maisha yajao.
"Embu jiandaeni kwa sababu maisha ni haya haya kila kitu Mungu ndio anaandika," ameongeza.
Kwa upande wa Mkuu wa shule hiyo, Jeremia Kitiku amesema shule hiyo imeshika nafasi ya kwanza katika mkoa huo katika matokeo ya kidato cha sita.
Amefafanua kuwa daraja (Division) la kwanza wanafunzi 162, daraja la pili wanafunzi 42, daraja la tatu wanafunzi wanne huku kukiwa hakuna daraja la nne wala zero.
Amesema matokeo hayo yanatokana na ari ya wanafunzi kujituma katika masomo, ushirikiano mkubwa kati ya wanafunzi, walimu, wazazi na viongozi katika wilaya hiyo, kufanya mitihani mingi ya maandalizi na motisha kwa wanafunzi na walimu wanaofanya vizuri kimasomo.
Aidha, amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa shule hiyo imekuwa na ongezeko kubwa la miundombinu na kukarabati sehemu kubwa ya majengo ya shule, hivyo kuwa msingi wa kupanda kwa ufaulu mwaka hadi mwaka.
Shule ya Sekondari Lulumba ilianzishwa mwaka 1990 ikiwa na kidato cha kwanza huku mwaka 2011 ikianza kupokea wanafunzi wa kidato cha tano kwa tahasusi ya PCM na PCB.