SGR KUIUNGANISHA TANZANIA NA NCHI JIRANI


Na HEMEDI MUNGA 

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa, amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake zote alizozifanya katika ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR).

Akizungumza katika kipindi cha Songa na Samia, Kadogosa amesema  ni juhudi kubwa sana za Mhe. Rais Dk. Samia kwa mradi huo ambalo unahitaji fedha nyingi kwa kuhakikisha wanaendelea mpaka kieleweke.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Zuhura Yunus, amesema mradi wa SGR  ni mfumo wa reli inayojengwa nchini kwa lengo la kuiunganisha Tanzania na nchi za  jirani kutoka Bandari ya Dar es Salaam hadi bandari ya Ziwa Victoria jijini Mwanza.

Nchi jirani zitakazounganishwa na SGR ni pamoja na Rwanda, Zambia, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia Congo (DRC)

Amsema Rais Dk. Samia ameendelea kutekeleza ahadi yake kwa Watanzania na kusimamia mwendelezo wa reli hiyo iliyoanza mwezi Aprili, 2017.

Amebainisha kuwa mradi huo unalenga kupunguza gharama za usafiri, muda wa kusafiri, urahisi wa kufikisha huduma mbalimbali za jamii na uwezeshaji wa biashara kati ya Tanzania na nchi za jirani.

Ameongeza SGR ni miongoni mwa miradi mikubwa katika historia ya Tanzania na Afrika Mashariki uliogharimu dola za Kimarekani bilioni 10.016 sawa na sh trilioni 23.3.

Amefafanua reli hiyo inapitia miji ya Dar es Salaam, Morogoro, Makutopora- Dodoma, Tabora, Isaka - Shinyanga, Mwanza, Rusomo-Rwanda, Bujumbura-Burundi, Goma-DRC na Kampala nchini Uganda.

Hata hivyo, Zuhura amedokeza mradi huo unatarajiwa kuleta manufaa mengi ambayo ni uwezeshaji wa biashara, kuchagiza  shughuli za kiuchumi, kurahisisha shughuli za kitalii, kuimarisha mahusiano ya kikanda na kupunguza muda wa safari huku ukifanikiwa kuongeza ajira na pato la Taifa.

Amesema hadi hivi sasa SGR imefanikiwa kutoa ajira za moja kwa moja 30,176 na ajira zisizo za moja kwa moja 150,388 na kufanikiwa kuzalisha pato la Sh. bilioni 358.75.

Naye, Mkurugenzi wa Ujenzi na Miundombinu wa TRC, Machibya Shiwa, amethibitisha mifumo ya mawasiliano, njia na vifaa vimekidhi viwango huku akieleza  kuwa Stesheni zote kutokea jijini  Dar es Salaam hadi Morogoro zimekamilika kwa aslimia 100.

Amesema wamezingatia viwango vyote vya kimataifa ikiwemo vile vya watu wenye mahitaji maalumu bila kuhitaji usaidizi mkubwa.

Akizungumza kuhusu kipande cha  kilometa 300 kutoka  Dar es Salaam hadi Morogoro kinachosubiriwa kwa hamu na wananchi, Naima Rajabu amesema walikua na hamu kubwa ya ujio wa treni ya kisasa.

Amesema treni za awali zilikua na changamoto sana ikiwemo watu kuchukua siku hadi tatu, hivyo mfumo wa wafanyabiashara kuwa mzito kutokana na hali ya usafiri.

"Ninaona treni hii ikija  mfumo wa biashara na uchumi utakua na maendeleo makubwa kwa sababu watu watakua wanasafiri kwa wakati na wanarudi kwa wakati, hivyo tunaiomba na tunashukuru, ije tunahamu nayo sana," amesisitiza Naima.

TRC imepokea vichwa vya treni vinne na mabehewa ya abiria zaidi ya 60 huku vichwa hivyo vya umeme vikiwa na kasi ya juu kwa kutumia kilometa 160 kwa saa.

Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imeweka historia barani Afrika kwa sababu SGR ni mradi pekee wenye kilometa 2010 unaotumia umeme.