WENYE MATATIZO YA MDOMO SUNGURA KUFANYIWA MATIBABU BURE MIKOA MINNE



 MWANDISHI WETU

TAASISI ya Qatar Charity na Al Ataa Charitable Foundation, kuwafanyia operesheni watoto 250 wenye tatizo la mdomo sungura, bila malipo katika mikoa minne.

Akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam, juzi, Mkurugenzi wa Al Ataa Charitable Foundation, Ahmed Elhamrawy, alisema huo ni utaratibu wao wa kufanya kambi za afya katika nchi mbalimbali duniani.

Amesema huduma hiyo ya operesheni mdomo wa sungura kwa watoto wenye tatizo hilo watafanyiwa bure katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Kigoma na Dodoma katika hospitali watakazopangia.

Elhamrawy amesema taasisi hiyo inazingatia masuala ya afya hususan katika matatizo ya macho, mdomo sungura na matatizo mengine ya afya, hadi sasa wameshafanya kambi 19 macho katika mikoa ya Dodoma, Pwani na Lindi.

Naye Mtaalamu wa Afya wa Qatar Charity, amesema wamekuja nchini kutoa matibabu hayo baada ya kupata data za kuwepo kwa watoto wenye matatizo ya mdomo sungura.

Amesema  matatizo hayo ya mdomo sungura yapo duniani kote, ndiyo maana madaktari wa Qatary 10 wanafanya kambi nchini Bangladesh na kundi hilo hilo April mwaka huu litahamia Ghana kuendelea na kambi kama hiyo.

Kwa upande wa Mratibu wa miradi ya Afya kutoka Al Ataa Charitable Foundation, Abubakar Rajab, amewataka wananchi wenye watoto wenye matatizo ya mdomo sungura wasiwafiche na badala yake wawapeleke hospitali wakafanyiwe operesheni.

"Wananchi wasiwafiche watoto wenye matatizo ya mdomo sungura kwa kudhani kuwa matatizo yanayotokana na ushirikina,  matatizo haya yapo duniania kote, jitokezeni mfanyiwe operesheni bure," amesema.

Rajab amesema matibabu yanatolewa bure kuanzia kugharamiwa usafiri kwa watakaokuwa mbali na vituo vya kutoa huduma, dawa zote ni bure pamoja na hiyo operesheni.