BARABARA YA ZIMBILI-KICHANGANI SEGEREA KUJENGWA KWA KIWANGO CHA LAMI


Na MWANDISHI WETU

Mbunge wa Jimbo la Segerea, wilayani Ilala, Jijini Dar es Salaam, Bonnah Kamoli, amesema dhamira  yake ni kuhakikisha barabara katika jimbo hilo zinapitika wakati wote ikiwa ni pamoja na kujengwa kwa kiwango cha lami, zege au changarawe.

Hayo yameelezwa leo katika hafla ya  Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) Wilaya ya Ilala, kukabidhi mradi wa ujenzi wa Barabara ya Zimbili-Kichangani ya Kilomita 0.5 kwa Mkandarasi Kampuni ya SERC Constructions Co.Ltd, Kata ya Kinyerezi.

Akizungumza kwa niaba ya Mbunge Bonnah, Katibu wa mbunge,  Lutta  Rucharaba,  amesema ujenzi wa barabara hiyo ni mwendelezo  wa utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na azma ya mbunge  huyo,  kuhakikisha barabara katika jimbo hilo zinakuwa bora.

Rucharaba amesema, Mbunge  Bonnah ana dhamira ya dhati  kuondoa changamoto ya barabara katika jimbo hilo kuhakikisha zinapitika wakati wote na zinajengwa kwa viwango na ubora hususan kiwango cha lami, hivyo kuwataka wananchi kutoa ushirikiano.

“Pia Mbunge anataka  ujenzi wa barabara hii ukamilike kwa wakati na ikiwezekana kabla ya muda. Vilevile Mbunge anataka  vijana wa eneo hili wapate ajira katika miradi hii.Kwa sababu hii miradi ni fursa pia ya ajira,”amesema Rucharaba.

Kwa upande wa Diwani wa Kata ya Kinyerezi, Leah Mgitu, ameipongeza  serikali  chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na Mbunge Bonnah, kwa ujenzi wa barabara hiyo kiwango cha lami  na kuomba Barabara ya Zimbili- Shule kujengwa kwa kiwango hicho pia.

  Meneja wa TARURA Ilala, Mhandisi John Magori, amesema,  gharama za mradi huo ni Sh. bilioni 1.3 na mradi unatarajiwa kukamilika   Septemba 11 mwaka huu na ujenzi tayari umeanza.

Magori, amesema mbali na kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami pia  mradi huo utahusisha ukarabati wa Barabara ya Zimbili  Kilometa 2.7  kwa kiwango cha changarawe.

Naye Mhandisi wa Kampuni ya SERC,  Justine Joseph, amesema watafanya kazi kwa viwango na kukamilisha mradi kwa wakati kwani wana uzoefu wa kutekeleza miradi.

Pia Uongozi CCM  Kata ya Kinyerezi, umemshukuru Rais Dk. Samia, mbunge, diwani na viongozi wa wilaya na mkoa wa Dar es Salaam,  kwa ujenzi wa barabara katika jimbo hilo hususan katika kata hiyo na kuomba  ujenzi huo uendelee kwa barabara zaidi hususan zinazopita katika makazi ya watu wengi.