DC MWENDA: WANANCHI FANYENI MAZOEZI KUIMARISHA AFYA



Na HEMEDI MUNGA 

WANANCHI na watumishi mbalimbali wilayani Iramba mkoani Singida wameaswa kuendeleza tabia ya kufanya mazoezi ya aina mbalimbali kwa lengo la kuendelea kutunza afya zao.

Akizungumza  baada ya mazoezi yaliyowakusanya watumishi wa mkuu wa wilaya, NMB, Makao Makuu ya Halmashauri, Walimu Wakuu, Polisi, Magereza na baadhi ya wananchi yaliofanyika leo katika viwanja vya Mabatini mjini Kiomboi wilayani hapa, Mkuu huyo wa wilaya, Suleiman Mwenda amesema mazoezi ni afya na ni njia kuu  ya kurefusha uhai wa mtu.

Aidha, ameipongeza Benki ya NMB kwa kuja na mpango huo wa kukimbia na kufanya mazoezi ya viungo yenye lengo la kufikisha taarifa na kuhamasisha wananchi kujiunga na benki hiyo na kutumia huduma mbalimbali ambazo inazitoa.

"Hakika mazeozi haya tuliyoyafanya yameimarisha na kuboresha miili yetu," amesema.

Ameeleza kuwa anaamini wakati wanaanza na walivyomaliza kutakua na mabadiliko makubwa katika miili yao.

Pia, amesema wamefanikiwa kukimbia takribani kilometa 10 licha ya wengine kukata moto mapema ingawa wameweza kufika katika kiwanja hicho.

" Ni jambo la kushukuru sana, nitoe wito tuendelee kufanya mazoezi kuimarisha na kuboresha afya zetu," ametoa wito DC Mwenda.

Kwa upande wa Kaimu Meneja wa Kanda wa benki hiyo, Emmanuel Kishosha amemshukuru Mkuu huyo wa wilaya kwa namna alivyoshiriki kikamilifu katika mazoezi hayo.

Aidha, amewapongeza washiriki wote kwa kujitoa kwao tangu asubuhi kwa sababu wamekua wakifanya mazoezi pamoja, hivyo wao ni mabingwa.

Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda, akiwaongoza watumishi mbalimbali kufanya mazoezi ya viungo yaliondaliwa na Benki ya NMB katika kiwanja cha Mabatini mjini Kiomboi,   wilayani humo, mkoani Singida. (Picha na Hemedi Munga)