Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Tulia Ackson, amewataka wanachama wa umoja huo kudumisha misingi ya IPU, ikiwemo kuendeleza amani na usalama, kulinda misingi ya demokrasia, kuchagiza Mabunge jumuishi, kulinda usawa wa kijinsia na kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
Dk. Tulia ameyasema hayo wakati akifunga Mkutano Mkuu wa 148 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) uliofanyika katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Geneva (CICG), nchini Uswisi.
Aidha, amesema viongozi wa Mabunge wanachama kuona umuhimu wa kutoa taarifa za utekelezaji ndani ya Mabunge yao juu ya maazimio ya Mikutano Mikuu yanayopitishwa ili kuleta matokeo chanya kwa jamii wanayoiwakilisha.
Dk. Tulia amesema IPU ni sehemu pekee ambayo Mabunge yanakutana kwa pamoja kupitisha maazimio yanayoihusu dunia na hivyo ni muhimu kwa Maspika wa Mabunge wanachama kuhudhuria Mikutano ya Umoja huo.
Mkutano wa 148 umehitimishwa na ulihudhuriwa na takribani misafara ya Mabunge zaidi ya 145.