WANANCHI WA IRAMBA WAMSHUKURU RAIS DK. SAMIA KWA KUWAPELEKEA FEDHA ZA MIRADI YA MAENDELEO

Na HEMEDI MUNGA 

 IRAMBA - SINGIDA 

Mkuu wa Wilaya ya Iramba, mkoani Singida,  Suleiman Mwenda amemuomba Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba kumfikishia salamu Rais Dk. Samia Suluhu, kuwa wanamshukuru kwa kuwaletea fedha zaidi ya sh bilioni 83.7.

Mwenda ametoa wito huo, katika Kijiji cha Nselembwe Kata ya Shelui wilayani humo, wakati akitoa ushuhuda mbele ya Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba kuhusu  miradi lukuki ambayo Rais Samia ameitekeleza katika wilaya hiyo.

Amesema wananchi wa wilaya hiyo waendelee kutembea kifua mbele kwa sababu Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ndani ya  miaka mitatu kila eneo la nchi hii amehakikisha  kuna miradi  ya maendeleo ambayo inatoa huduma karibu ya wananchi.

"Ninawahakikishia ndugu zangu Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kubwa sana, hivyo tunakila sababu ya kuendelea kumuunga mkono na kumuombea aendelee kua na afya njema kwa lengo la kuendelea kuwatumikia wananchi," amesema.

Pia, amesema  kwa mara ya kwanza serikali ya Rais Dk. Samia,  imevunja rekodi kwa kutengeneza barabara za ndani kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) ambapo  bajeti iliyokua inakuja ni sh milioni 500 na zilikua hazifiki zote huku katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wake aliwaletea sh bilioni 8.2.