WAALIMU 336 WA SHULE ZA SEKONDARI WILAYANI MSALALA WAPATIWA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO WANANFUNZI

MWAKILISHI wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, William Chungu, akizungumza katika kufunga mafunzo ya kuwajengea uwezo waalimu wa Shule za Sekondari wilayani Msalala, Mkoa wa Shinyanga, yaliofadhiliwa na Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, wilayani humo, mwishoni mwa wiki.  (Na Mpigapicha Wetu).

 

Na MWANDHISHI WETU

WAALIMU 336 wa shule za sekondari wanaofundisha masomo ya sanaa na Lugha, katika Wilaya ya Msalala, wamepatiwa mafunzo maalumu kuhusu namna ya kufundisha na kuwajengea umahiri wanafunzi.

Akizungumza katika kufunga mafunzo hayo, mkoani Shinyanga, mwishoni mwa wiki,  Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Khamis Katimba, alisema baada ya mafunzo hayo wanatarajia kuona utofauti wa ongezeko la ufaulu katika shule zote za Halmashauri hiyo.

Amesema mafunzo hayo yaliofadhiliwa na mgodi wa Barrick Bulyanhulu, yatasaidia kuinua kiwango cha elimu ya sekondari kwa kuongeza ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya taifa ya kidato cha pili na nne, wilayani humo.

Katimba amewataka hao waliopata mafunzo hayo yakalete tija kwa wanafunzi na wakawe wazazi katika hizo shule na kuhakikisha unyanyasaji wa kinjisia hautakiwi kwa wanafunzi wao.

“Nichukue Nafasi hii kuwapongeza ndugu zetu wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu kwa kazi kubwa mnayoifanya hasa kwa kushirikiana na serikali katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo", alisema.

Kwa upande wake, Ofisa Elimu wa Halmashauri ya Msalala, mkoani Shinyanga, Seleko Ntobi, amesema mafunzo hayo ni muhimu na yanamanufaa makubwa katika sekta ya elimu na kuleta tija.

"Tumepata mafunzo kutoka kwa timu ya wakufunzi wabobezi kutoka Chuo cha Ualimu Shinyanga (SHYCOM), ambao wamekuwa msaada mkubwa sana kwa walimu wetu, kabla ya mafunzo haya walikuwa hawana uelewa unaofanana katika kufundisha na kupima kwa kuzingatia umahiri wa wanafunzi", amesema.

Naye Mwakilishi wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, William Chungu amesema, Barrick itaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali kuboresha maisha ya wananchi hususani katika sekta za elimu na afya. 

"Tunafurahi jinsi Serikali inavyofanya jitihada za kuboresha maisha ya wananchi, nasi wawekezaji tutaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali husuani katika suala la elimu ukiwemo, mradi wa ujenzi wa miundombinu ya shule, kuwawezesha wanafunzi kusomea katika mazingira rafiki", amesema.

Pia Chungu amesema Barrick Bulyanhulu, imekuwa ikitekeleza Mpango wa kuinua ufaulu shuleni wa wanafunzi wa sekondari (PIP), kwa kushirikiana na Halmashauri za Nyang’hwale na Msalala kwa lengo la kupata matokeo mazuri kwa kuongeza idadi ya ufaulu wa wanafunzi katika wilaya hizo, kupitia fedha za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) zinazotolewa na mgodi huo.