DC MWENDA: WENYE NIA YA KUPATA UONGOZI WA JUU WAKUMBUSHWA KUMUELEKEA MUNGU

Mkuu wa Wilaya ya Iramba, mkoani Singida, Suleiman Mwenda, akizungumza wakati wa dua ya kumuombea Rais Mstaafu wa Awamu ya pili, Hayati Ali Hassan Mwinyi, katika Msikiti wa Taqwa, mjini Kiomboi wilayani homo. (Picha na Hemedi Munga)

Na HEMEDI MUNGA

NAFASI ya uongozi wa urais nchini  ni nafasi ambayo ni nzito na ngumu, hivyo wenye malengo ya kukipata cheo hicho wamekumbushwa kumuelekea Mwenyezi  Mungu  kwa lengo la kumuomba ridhaa ya kuiongoza jamii.

Akizungumza baada ya dua ya kumuombea Rais wa Awamu ya Pili, Hayati  Ali Hassan Mwinyi iliyofanyika katika  Msikiti wa Taqwa mjini kiomboi wilayani Iramba mkoani Singida, Mkuu wa wilaya hiyo, Suleiman Mwenda amekumbusha kuwa suala la urais ni jambo zito na gumu linalohitaji msaada wa Mungu.

Mwenda amesimulia wosia aliowahi upata kutoka kwa rafiki yake aliyetambulika kwa jina la Mwinyi baada ya kumtembelea rais huyo nyumbani kwake enzi za uahi wake baada ya kustafu.

Ameeleza kuwa wakati wakiwa wanosoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) baadhi yao walimtembelea Rais Ali Hassan Mwinyi ambaye aliwauliza nini malengo yao hapo baadae watakapokua wamemaliza masomo yao.

Mwenda amesimulia kuwa  rafiki yake huyo, alimwambia Rais Ali Hassan Mwinyi kuwa anataka kua rais kama yeye.

Kauli hiyo ilifanya Rais Ali Hassan Mwinyi kumueleza kijana huyo kuwa lengo lake aliloliweka ni kubwa sana.

"Hakika umeazimia jambo gumu sana, ikiwa azma yako ipo katika nafasi yako, basi kuanzia leo hii kila siku usiku simama uzungumze na Mwenyezi Mungu, mueleze na kumuomba akusaidie mpaka utakapokua Rais," amenukuu maneno ya Rais huyo DC Mwenda.

Amesema kuwa Rais Ali  Hassan Mwinyi alimwambia kijana huyo,   jambo la urais ni zito na gumu linalohitaji uwezo wa kipekee wa Mwenyezi Mungu.

Aidha, ameongeza kuwa ni Mwenyezi Mungu pekee hua anapanga ni nani katika waja wake awe kiongozi wa wenzake katika jamii.

Hata hivyo, Mwenda amesema kuwa  alijifunza kutoka kwa Rais huyo, uadilifu, utii, unyenyekevu na uchamungu wa kweli kuwa ndio njia sahihi katika nyanja mbalimbali za maisha na uongozi.

Amewataka  watu wanapoweka azma ya kufanya jambo lolote hususan lilanogusa jamii au kundi fulani ni vizuri kujielekeza kwa Mwenyezi Mungu kwa lengo la kupata ridhaa ya uongozi.

" Mzee wetu Ali Hassan Mwinyi wakati wote alimuelekea Mwenyezi Mungu licha ya misukosuko aliyowahiipitia katika uongozi wake," amesema Mwenda.

Amebainisha kuwa  licha ya Misukosuko hiyo, bado aliweza kuiongoza nchi kwa mafanikio makubwa katika nyanja mbalimbali ikiwemo biashara huria, utawala na dilpomasia.

Rais Dk. Samia Suluhu Hassan alitangaza  kifo cha Hayati Rais Ali Hassan Mwinyi Februari 29, 2024 na atazikwa Machi 02, 2024.