BALOZI DK. NCHIMBI ATOA MAAGIZO KWA TAMISEMI KUANZA UJENZI WA KITUO CHA AFYA NGIMU

SINGIDA DC - SINGIDA 

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, kuanza ujenzi wa kituo cha afya  Ngimu ifikapo  Agosti  15, 2024.

Dk . Nchimbi ametoa agizo hilo wakati aliposimama kuwasalimia wananchi wa Kata  ya Itaja wilayani Singida DC, mkoani Singida akiwa ziarani kuelekea mkoa wa Manyara baada ya kumaliza ziara mkoani humo.

Aidha, amewaahidi wananchi hao ifikapo tarehe 20 ya mwezi huo yeye, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi na Uenezi, Amos Makala na Katibu wa NEC Idara ya Mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI), Rabia Abdallah Hamid, watakuja kukagua ujenzi huo.

"Kwakua alikuja Katibu Mkuu wa Chama akaahidi kitajengwa ndani ya miezi mitatu na hakijajengwa hadi sasa, ninamwambia Waziri wa TAMISEMI nataka kituo hichi kianze kujengwa mwezi Agost 15, shuguli ianze moto moto," amesema Dk. Nchimbi.