Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezitaka mamlaka zinazohusika na usimamizi wa sekta ya habari ziendelee kusimamia vyombo vya habari vizingatie maadili na kujiepusha na uchapishaji wa taarifa na picha zinazochochea uvunjaji wa maadili, mila na desturi za Kitanzania.
Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa habari za mitandao ya kijamii na vyombo vya habari ili kuhakikisha kuwa sekta hiyo inaendelea kukua na kuchangia kuleta maendeleo kwa Taifa.
“Kupitia vyombo vya habari, hasa vya mitandao ya kijamii, tumeweza kuwahabarisha wananchi kuhusu shughuli na mipango ya Serikali, na kuhamasisha ushiriki na ushirikishwaji wa wananchi katika shughuli na mipango hiyo.”
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Mei 21, 2024) katika Kongamano la Jumuiya ya Wanahabari wa Mitandaoni ya Kijamii (JUMIKITA) kuhusu mafanikio ya miaka mitatu ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwenye Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Ameongeza kuwa Serikali imechukua hatua mbalimbali katika kuboresha Sheria na Miongozo inayosimamia sekta ya habari ili kuweka mazingira wezeshi kwa wanahabari kufanya kazi zao kwa uhuru na kwa kuzingatia maadili, tamaduni na haki za watu wengine.
“...Katika kipindi hiki cha miaka mitatu toka Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aingie madarakani amewezesha kukua kwa sekta ya habari na hasa ongezeko la watumiaji na wasomaji wa habari kupitia mitandao ya simu.”
Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali imeandaa Mkakati wa Mawasiliano wa Taifa ili kuhakikisha wadau katika ngazi zote wanapata taarifa za kutosha na wanashiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi na kuimarisha mawasiliano ya Serikali.
Awali, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ameilekeza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) iandae utaratibu wa kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa waandishi wa habari za mitandaoni ili kuwajengea uwezo wa kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadili na utamaduni wa Kitanzania.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa JUMIKITA, Shaban Matwebe ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ilivyosimamia ukuaji endelevu wa sekta ya habari nchini ikiwemo kuimarisha uhuru wa vyombo hivyo.