DIWANI HASSAN AIPONGEZA CCM KWA KUSIMAMIA UTEKELEZAJI WA ILANI YA CCM KATIKA MTAA WA KIZEGA, WILAYANI IRAMBA
![]() |
| Diwani wa Kata ya New Kiomboi wilayani Iramba mkoani Singida, Omari Hassan. |
Na HEMEDI MUNGA, Iramba
Diwani wa Kata ya New Kiomboi wilayani Iramba mkoani Singida, Omari Hassan na wananchi wa Mtaa wa Kizega katika Kata hiyo wamesema hawana deni na Chama cha Mapindunzi (CCM) ambacho kinaongozwa na Mwenyekiti wake Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kutokana utekelezaji wa Ilani ya CCM.
Akizungumza na wananchi na baadhi ya wanachama wa chama hicho, katika Mtaa huo, Diwani wa Kata hiyo, Omari Hassan ameweka wazi mambo yote waliyoahidi kupitia Ilani ya chama hicho ikiwemo barabara, umeme na maji yametekelezwa kwa zaidi ya asilimia 90.
Amesema katika kipindi chake mtaa huo umepata Sh. milioni 600 kwa lengo la kujenga shule ya sekondari mpya, barabara yenye thamani ya Sh. milioni 450 na mradi wa maji wa Sh. milioni 70 vikitekelezwa kwa asilimia 100.
Hassan amesema eneo la Kizega linakuwa kwa kasi hiyvo wanao mradi wa miji 28 na kuchimba visima vitatu Ruruma, vitakavyoendelea kuhakikisha maji yapo muda wote.
Ameeleza kipindi cha nyuma barabara ya Kizega ilikua haipitiki huku Chama hicho kupitia serikali yake ilitengeneza barabara hiyo kwa kiwango cha Changarawe na lakini sasa hivi inapitika.
Pia, amesema baada ya wananchi kutoa ardhi yenye hekta 21 kwa lengo la kujenga shule tayari Rais Dk. Samia ameagiza Sh.milioni 600 kujenga shule hiyo.
Hassan amesema kuhusu namna ilivyopatikana shule hiyo baada ya kumfahamisha mbunge wa Jimbo hilo ambae ni Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, alielekeza likajadiliwe katika vikao vya madiwani na kupitishwa.
"Tunamshukuru Rais wetu Dk. Samia kwa kutuona na tunamuhakikishia hatuna deni naye, kazi yetu tunasubiri muda tu, tumuoneshe upendo wetu kupitia sanduku la kura," amesema.
"Tuendelee kujiandaa na kutafakiri kwa kina kulipa wema ambao viongozi wetu wametufanyia na tusiingize mabakamabaka katika kata yetu."
Aidha, Hassan amebainisha kata hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu ya Rais Dk. Samia ilipokea Sh. bilioni 3.8 fedha ambazo zilitolewa kwa wilaya nzima kipindi cha nyuma, lakini leo hii ni fedha zilizotekeleza miradi mbalimbali katika kata hiyo.
"Niwaombe ndugu zangu mwanga tunaouona tusiubedhe wala kuuchafua kwa sababu tukiuzima tutakwenda kwenye giza ambalo litatugharimu miaka mingi Tanzania ni kubwa kuliko Iramba, hivyo tusijinyanyase wenyewe, tuendelee Kuiamini CCM," amesema.
Amesema mema na mazuri waliyoyapata hawana deni na CCM, hivyo wataendelea kukiamini Chama ambacho ni mwarobaini wa kuendelea kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi.
Kwa upande wa Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya hiyo, Yusta Lisu, amewaomba wananchi hao waendelee kumuunga mkono Rais Dk. Samia kwa kuwa ameendelea kuwapigania wananchi wake wapate maendeleo.
"Tuendelee kumuombea Rais wetu kila siku anaendelea kuiangalia Iramba kwa jicho la tatu kwa sababu maendeleo anayotupa sio mazingaombwe tunayaona, wenyewe," amesema.
Yusta amewahakikishia wananchi hao kuhusu barabara za mtaa huo na kwingineko kupitia bajeti ya 2024 hadi 2025 zitajengwa kwa kiwango cha lami yakati.
"Tumlipe nini huyu Mama ! hakika tumpe haki yake kwa sababu ndani ya miaka mitatu ya uongozi wake tunatembea kifua mbele," amesema.
![]() |
| Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya hiyo, Yusta Lisu. |
Reviewed by Gude Media
on
June 04, 2024
Rating:

