WATU WENYE ULEMAVU, VIJANA NA WANAWAKE HAMASISHENI WANANCHI WAJITOKEZE KATIKA UBORESHAJI WA DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA:INEC

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji (RUFAA) Jacobs Mwambegelee

Na MWANDISHI WETU, Dar es Salaam

Tume Huru ya Taifa ya Uchagzui (INEC), imewaomba watu wenye ulemavu, vijana na wanawake, kuwahamasisha wananchi kujitokeza katika kujiandikisha au kuboresha taarifa zao katika uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.

Akifungua mkutano wa tume na wawakilishi wa vijana, Dar es Salaam, Mwenyekiti wa INEC, Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele, amesema wameanza mchakato wa uboreshaji wa daftari, ambapo utazinduliwa mkoani Kigoma Julai o1, 2024, mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Amesema uboreshaji huo unawahusu wananchi wenye sifa za kuandikishwa kuwa wapiga kura na anayeboresha taarifa zake, hivyo kuwakumbusha wananchi kupitia majukwaa mbalimbali wajitokeze kujiandikisha na kuboresha taarifa zao.

"Kwenye uboreshaji wa daftari yaliyopita, vijana mmekuwa msaada mkubwa katika kuhamasisha na kuelimisha wananchi haswa vijana kupitia majukwaa mbalimbali, hususan mitandao ya kijamii", amesema.

Mwambegele amesema uboreshaji wa daftari wa mwaka 2024/25, utatumia teknolojia ya BVR Kits zilizoboreshwa kwa kuwekwa programu endeshi ya kisasa, pia BVR Kits zitakazotumika zimepunguzwa uzito ambapo zitakuwa rahisi kubeba na kurahisisha zoezi hilo katika maeneo ya vijijiini.

Amesema tume katika kuhakikisha inaenda na mabadiliko ya teknolojia imeboresha mfumo wa uandikishaji, utamwezesha mpiga kura aliyepo katika daftari, kuboresha taarifa zake au kuhama kituo kwa kutumia simu au kompyuta na baadaye kutembelea kituo anachokusudia kujiandikisha apatiwe kadi yake ya mpiga kura.

Pia Mwambegele amewataka vijana,  kuwakumbusha vijana wenzao kuendelea kuzingatia sheria za uchaguzi, kanuni za uboreshaji na maelekezo ya tume kuhusu uboreshaji wa daftari.

Amesema tume kwa upande wao watazingatia katiba, sheria ya uchaguzi na kanuni zilizotungwa chini ya sheria katika zoezi hilo la uboreshaji.

Wawakilishi wa watu wenye ulemavu wakiwa katika mkutano na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
Wawakilishi wa vijana wakiwa katika mkutano na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC). 

Wawakilishi wa Wanawake wakiwa katika mkutano na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).