MARTHA: WANANCHI KATAENI WANASIASA WANAOTOA KAULI ZENYE VIASHIRIA VYA UVUNJIFU WA AMANI

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Singida, Martha Mlata.

Na HEMEDI MUNGA, Iramba 

Wananchi na wanachama wa CCM wilayani Iramba mkoani Singida, wameombwa kuwakataa viongozi wa kisiasa wanaodaiwa kutoa kauli za kichochezi, kibaguzi na zenye viashiria vya kuvunja amani.

Akizungumza na wananchi katika Uwanja wa Stendi ya mabasi mjini Kiomboi, wilayani humo, Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa huo, Martha Mlata, amesema wapuuze maneno yoyote yanayosemwa kwa lengo la kutaka kuwapotosha na kuwadanganya watu.

Martha amesema wananchi waendelee  kumuombea na kumuamini Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambae amejitoa kuwaletea maendeleo katika nyanja zote ikiwemo maji, umeme, barabara na elimu.

Amesema adha ya usafiri waliokuwa wakiipata wananchi huko nyuma, ambapo walilazimika kutoka Iramba kwenda kupanda gari Singida mjini kuelekea Dar es Salaam, lakini leo hii mabasi yanaanzia safari mjini Kiomboi kwa sababu ya uwepo wa barabara za lami.

Martha amesema wanafunzi walilazimika kutumia vibatali wakati wa kujisomea ambavyo viliingiza moshi puani hali ambayo hivi sasa haipo kwa sababu Rais Dk. Samia amefikisha umeme katika vijiji vyote, hivyo wanakila sababu ya kuendelea kumuunga mkono.

Kuhusu elimu ameeleza watu walikua wanafaulu lakini anayepata bahati ya kuendelea na masomo anachaguliwa mmoja tu, hivi sasa shule zimejengwa katika kila kata kwa kutumia zana za kisasa.

Akizungumzia kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Martha amesema ni tunu ya Taifa, wazee wao waliungana kwa sababu walikua wanataka kuleta maendeleo.

"Ni lazima tuendelee kutunza amani ya Taifa hili kwa ajili ya vizazi vijavyo, hivyo wakija wakataeni," amesema.

"Viongozi wangu wa  dini niwaombe muendelee kumuombea Rais wetu Dk. Samia Suluhu Hassan na kumtaka anayejiita mchungaji anayetamka kuwa Rais amekataliwa na Mungu akatubie kwa kuwa yeye ndio amekataliwa na Mungu kwa kukosa weledi wa kuhutubia," ameomba.

Kwa upande wa Katibu wa CCM mkoa huo, Lucy Shee, amesema haikubaliki kwa kiongozi wa chama cha sisasa kuomba kibali cha kuhamasisha na kuimarisha chama chake halafu akiishapanda katika jukwaa anahubiri habari ya kuvunja Muungano.

Amesema Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema atakae anza kusema sisi watanganyika na wao wazanzibari lana itamtafuna ndio maana chama cha kiongozi huyo kinatafunwa na lana kwa sababu ya kutaka kuwarudisha Watanzania kwenye ukabila na ubaguzi wa kidini.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa Mkoa huo, Halima Dendego ametoa wosia anayemtukana Mama wa mwenzie na wakwake atatukanwa, anayemdharau Mama wa mwenzie na wakwake atadharauliwa na yoyote anayemdharau mwanamke katika dunia hii anahasara.

"Ndugu zangu muogopeni mtu wa namna hiyo alielala tumboni mwa Mama yake miezi tisa  halafu leo anasima hadharani kumtukana mwanamke bila woga, hakika huo ni ushetani na Watanzania hatuna tabia hiyo," amesema na kuongeza kuwa:

"Hatutakubali matusi, sio sehemu yake, tunatukanwa matusi wakati tumefanya mambo makubwa", amesema.

Amesema Watanzania hawana mila hiyo kwa sababu siasa ni kupishana kwa maendeleo kuwa wewe utafanya hivi kwa kutumia njia hii na mwingine atafanya hivi kwa kutumia njia ile na sio kutukanana.

Naye Mkuu wa wilaya hiyo, Suleiman Mwenda amesema hivi karibuni alipita kijana katika wilaya hiyo na kusema Rais hajafanya kitu, jambo ambalo sio kweli, amekosa hoja kwa sababu Rais Dk. Samia ameipendelea Iramba. 

Mwenda amesema zaidi ya sh bilioni 83.7 zililetwa na Rais Dk. Samia katika wilaya hii kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Mkoa wa Singida, Lucy Shee.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego