Korosho CUP Kuanza kutimua vumbi Agosti Jimbo la Lulindi Mtwara

Na MWANDISHI WETU

Ligi soka ya  Korosho  Cup  inatarajia kuzinduliwa Agosti 10  mwaka huu katika Jimbo la Lulindi, Masasi, mkoani  Mtwara huku zawadi nono zikitangazwa kwa washindi.

Mwandaaji na Mdhamini wa  ligi hiyo ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya  Utalii 255 Community,  Angelina Malembeka, amesema, bingwa atazawadiwa  pikipiki ya magurudumu  matatu maarufu kama  guta yenye thamani ya sh. 6,000,000, kombe, jozi moja ya jezi, mpira mmoja na fedha taslimu sh. 100,000 za mafuta.

Malembeka,  amesema,mshindi  wa pili  atapata kitita cha sh. 1,000,000, jozi moja ya jezi na mpira mmoja, huku mshindi wa watu  akiondoka na sh.500,000 na  mshindi wa nne  akipata sh. 200,000.

“Golikipa bora  atazawadiwa shilingi 50,000, mfungaji bora shilingi 50,000, kocha bora shilingi 50,000 na mwamuzi  bora shilingi 50,000", amesema.

Malembeka  ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu akiwakilisha  Mkoa wa Kaskazini Unguja,  ameeleza  kundi bora la ushangiliaji  litaondoka na kitita cha sh.100,000.

“Timu zote zinazoshiriki zitapewa jezi jozi moja na mipira miwili. Waamuzi wote watapewa sare,”amesema.

Amebainisha,  ligi hiyo itatimua vumbi katika vituo  vitatu  ambavyo ni  Kata ya Namwanga, Kata ya  Chiungutwa na Kata ya Mchauru.

“Kila kituo  tutakipa  filimbi, kadi nyekundu na njano, kibao cha kubadilisha wachezaji, pampu ya kujaza mpira, nyavu za golini na beji za makapteni,”amebainisha.

Amesema  kaulimbiu ya michuano hiyo  inasema ni Shiriki Uchaguzi  wa Serikali za Mitaa 2024  ikilenga kuhamasisha wananchi wa Lulindi kushiriki uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.

Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Masasi,  kimebariki  michuano  hiyo  na kuwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi.

Mweka Hazina wa  chama hicho, Japhari  Lwenge, amesema ligi hiyo itashirikisha timu 14 kutoka kata 14 za Jimbo la Lulindi.

“Ligi itaanzia ngazi ya Kata kwa kushirikisha timu za mitaa kisha,  kila kata itatoa timu moja itakayoshiriki michuano hiii,”amesema Lwenge.