Na MWANDISHI WETU
MEYA wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Songoro Mnyonge, amewataka madiwani wa halmashauri hiyo kuzingatia kanuni za kudumu za halmashauri wanapokwenda kukagua miradi ya maendeleo.
Amesema ukaguzi holela wa miradi bila kuzingatia kanuni unaweza kuitumbukiza manispaa hiyo katika changamoto, kuzua taharuki na upotoshaji.
Mnyonge, ameyasema hayo Dar es Salaam, leo alipoongoza kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo.
Meya Mnyonge amesema kanuni ziko wazi na zinaelekeza diwani ni lazima atoe taarifa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri na ili apewe wataalamu watakao toa maelezo ya miradi husika.
“Sasa mimi ndiyo kungwi wenu hapa. Hakuna kungwi mwingine hapa zaidi yangu.Zingatieni kanuni. Mnamwita Naibu Meya kuja katika ziara kwenye kata zenu aje kufanya nini?”, amehoji.
Ameongeza Ibara ya 78 ya kanuni hizo za kudumu za halmashauri inatamka wazi kuwa Mjumbe wa Halmashauri anaweza kutembelea, eneo, jengo au shughuli za ujenzi zinazotekelezwa na au kwa niaba ya halmashauri na anaweza kutuma taarifa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri akieleza sababu za matembezi yake ili aweze kupangiwa watalaamu wa mradi au shughuli husika kwaajili ya kupata maendeleo ya kitaalamu,”.