Waziri Jafo atembelea FCC asisitiza bidii ya kazi na ufanisi wa ukaguzi kampuni

Na MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Viwanda na Biashara Dk.Seleman Jafo amesema Wizara hiyo inafursa kubwa kutengeneza ajira kwa Watanzania kupitia sekta binafsi ikiwemo viwanda, hivyo watahakikisha wanatimiza azma hiyo ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kuleta maendeleo kwa wanachi.

Waziri  Dk.Jafo ameyasema hayo jana Jijini Dar es Salaam, alipotembelea FCC kujitambulisha kwa viongozi wa Taasisi hiyo tangu ateuliwe na kuzungumza nao juu ya kazi kubwa wanayoifanya katika kulinda ushindani nchini.

Amesema Wizara hii ni pana na ina umuhimu mkubwa katika kutoa ajira kwa wananchi kupitia sekta binafsi, hivyo lazima tuhakikishe tunaweka mazingira mazuri kuongeza uwekezaji ambao unatoa ajira kwa Watanzania wengi.

Amesema kwa kazi kubwa iliyofanywa na Rais Dk.Samia, ndani ya miaka mitatu imechochea ongezeko la viwanda vikubwa kwa asilimia 27, ikiwa ni hatua kubwa ya ukuaji sekta hiyo na kuchochea ukuaji uchumi.

Akimshukuru Waziri Dk.Jafo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa FCC, Dk. Agrey Mlimuka, alimpongeza Waziri Jafo kwa kuwatembelea huku akiahidi kusimamia utekelezaji wa maagizo yote aliyoyatoa ikiwemo la kufanya ukaguzi wa miungano ya kampuni

Awali Mkurugenzi Mkuu wa FCC, William Erio, alimshukuru Waziri Dk. Jafo kwa ziara hiyo katika ofisi zao, huku akisema wako tayari kushirikiana naye kutimiza azma ya serikali.

Amesema FCC inafanya kazi kubwa ya kuhamasisha ushindani halali nchini, kudhibiti bidhaa bandia, kwa lengo la kulinda soko na kuvutia uwekezaji kwa uwepo mazingira bora ya biashara nchini.