Mwonekano wa jengo la Kituo cha Afya cha Msimbati, Mtwara. |
NA MWANDISHI WETU
SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), limeendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha huduma za kijamii, ambapo limetoa sh. bilioni moja kuinua sekta ya afya mkoani Mtwara.
TPDC inafanya hivyo, maeneo ambayo shughuli za utafutaji, uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa gesi asilia zinafanyika.
Huduma za kijamii zikiwemo afya, elimu, maji na utawala bora zinaimarishwa ikiwa ni sehemu ya Uwajibikaji wa Shirika kwa Jamii (CSR).
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa TPDC, Marie Msellemu amebainisha hayo mkoani humo.
"Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limetoa jumla ya shilingi bilioni moja kuinua sekta ya afya mkoani Mtwara, kati ya fedha hizo shilingi milioni 600 zimetolewa kwa ujenzi wa Kituo cha Afya Kijiji cha Msimbati na shilingi milioni 400 zimetolewa kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya Kijiji cha Nyundo, kilichopo Kata ya Nyundo, Wilaya ya Nanyamba," alisema.
Kwa upande wake, Mbunge wa Nanyamba, Chikota akizungumza na wananchi wa jimbo hilo, ameishukuru TPDC kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha sekta ya afya.