Mbunge Kanyasu amshukuru Rais Dk.Samia kutatua migogoro ya Madini Geita Mjini

Na MWANDISHI WETU

MBUNGE wa Geita Mjini, Costantine Kanyasu amemshukuru Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo ameendelea kutatua changamoto mbalimbali ya migogoro ya madini iliyodumu kwa muda mrefu hususan ule wa eneo la Samina uliokuwepo kwa zaidi ya miaka 20.

Kanyasu ameyasema hayo  Mkoani Geita, katika mkutano wa ufunguzi wa Maonesho ya Saba ya Teknolojia ya Madini, yaliyo udhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama na serikali wakiongozwa na  Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko.

" Tunamshukuru Rais Samia kupitia kwa Waziri wa madini, Antony Mavunde kwa usikivu wake na unyenyekevu wake wa kutatua migogoro  ya madini katika maeneo mbalimbali ikiwemo eneo la Samina lilochukua muda mrefu zaidi ya miaka 20," amesema.

"Tuna shukuru kwa hatua nzuri iliyofikiwa kaka alivyoeleza kiongozi wa GGM, kwamba watu wamelipwa fidia zao, wamejenga nyumba nzuri na zoezi la kuhama kutoka maeneo yale linaenda vizuri," amesema.

Amesema wanaendelea na mazungumzo katika maeneo ya Nyamalebo, Nyakabale , magema, ambapo wanapata matumaini kuwa yataenda vizuri, yataisha salama na kupata muafaka.