MHASIBU ALIYEDAI KUTEKWA NA KUIBA SH. 60 ANASHIKILIWA NA POLISI



Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, akizungumza na waandishi wa habari, kuhusu mtuhumiwa aliyetoa taarifa uongo za kuporwa na kujeruhiwa na majambazi na kuondoka Sh. milioni 60 za kampuni ya kichina ya Your Home Choice.


Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, inamshikilia Mhasibu wa Kampuni ya Your Home Choice, Deodatus Thadei Luhela, kwa kutoa taarifa za uongo katika kituo cha polisi za kudai kujeruhiwa na kuporwa fedha Sh. milioni 60.

Kamanda Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amesema fedha hizo alitumwa na mwajiri wake kuzichukua katika benki ya CRDB tawi la Tazara.

Muliro amesema mtuhumiwa huyo alidai asubuhi saa 3.00 alikamatwa na majambazi wawili waliokuwa na gari nyeusi baada ya kumtishia kwa silaha baadae akaingizwa katika gari na walimjeruhi mkono wa kushoto na shavuni na kumpora fedha alizokuwa nazo.

"Mtuhumiwa alidai alikamatwa na majambazi wakamjeruhi na kumpora fedha zote alizokuwa nazo na baadaye kumtupa maeneo ya Gongo la Mboto njia panda ya Pugu na Mbezi, alijikongoja hadi kituo cha Polisi kidogo cha Gongo la Mboto ambako alipewa PF. 3 kwaajili ya matibabu", alisema.

Amesema baada ya tukio hilo ilipofika saa 8.00 mchana, mtuhumiwa alifungua kesi kituo cha Polisi Chang’ombe ya unyang’anyi na kuporwa fedha Sh.milioni 60.

Muliro amesema makachero wa Polisi walimuhoji kwa kina na kubaini kuwa taarifa hizo zilikuwa ni za uongo, ambapo mtuhumiwa aliwapeleka askari hadi Chanika Kitunguu alipokuwa amezificha pesa hizo.

Pia Muliro amewatahadharisha wananchi kuhusu tabia ya kutoa taarifa za uongo kwa maofisa wa Serikali ni kosa na ikibainika watachukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria ikiwemo kufikishwa mahakamani.

Wakati huo huo, Polisi amemkamata Mkazi wa Kijitonyama, Joseph James, kwa kujifanya askari Polisi kutoka ofisi ya Upelelezi Makao Makuu ya Polisi Dodoma.

Muliro amesema uchunguzi umebaini mtuhumiwa huyo amekuwa akishirikiana na wenzake kufanya uhalifu kwa kutumia gari aina ya Subaru yenye namba za usajili T 550 DST alilokamatwa nalo mtuhumiwa huyo.

Amesema wanalifuatilia kundi la watu waojifanya ni askari Polisi wakati mwingine maofisa wa Usalama wa Taifa na kuwakamata watu hovyo, kuzunguka nao mitaani kwa kutumia gari huku wakiwatishia kuwapa tuhuma mbalimbali za uongo na baadaye kuwataka watoe pesa ndio wawaachie.

Muliro amesema polisi inaenedelea kuwasaka wahalifu wote wanaofanya utapeli wa namna hii ili wakamatwe na kufikishwa kwenye mifumo ya kisheria kwa hatua zaidi.


Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, akionyesha fedha zinazodaiwa kuibwa na mtuhumiwa aliyetoa taarifa uongo za kuporwa na kujeruhiwa na majambazi na kuondoka Sh. milioni 60 za kampuni ya kichina ya Your Home Choice.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, akionyesha fomu ya PF 3, kwa waandishi wa habari.