MCHINA ADAKWA NA POLISI KWA TUHUMA ZA MAKOSA YA KIMTANDAO

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, akionyesha vifaa vilivyokuwa vikitumika kuingilia mifumo ya mawasiliano na kusababisha hasara kwa Serikali pamoja na vifaa vya wamiliki wa luninga za mitandaoni.


Na Mwandishi Wetu

Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, kwa kushirikiana na timu maalumu ya kuzuia na kupambana na makosa ya mtandao,  imewakamata watuhumiwa 11 wa makosa ya kimtandao kufuatia  ufuatiliaji mkali unaoendelea kufanywa na Jeshi la Polisi na timu hiyo maalumu.

 Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amesema Jeshi la Polisi na timu hiyo, imemkamata Alex Magoti (26) Mkazi wa Tabora Mjini na wenzake nane kwa tuhuma za kumiliki luninga za mtandaoni na akaunti za mitandao ya kijamii.

Amesema luninga na akaunti za mitandao ya kijamii zimekuwa zikitumika kusambaza taarifa za uongo au uzushi kuhusu, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine wakuu wa Serikali.

Muliro amesema Watuhuhumiwa hao wamekuwa wakiweka taarifa zao za uzushi, uongo na upotoshaji kwenye luninga za mtandaoni zinazotambulika kwa majina ya BSUN Online TV, GATTU Online TV, TAMUTAMU online TV, KILIMANJARO online TV na nyinginezo.

Amesema mfano wa taarifa hizo ni kama 'Rais Samia akosoa vikali utawala wa Rais JPM, aanika ukatili aliofanya (haukubaliki hata kidogo)', 'IMEVUJA VIDEO, MBOWE APEWA SHAVU…!', 'DENI LA TAIFA LAIBUA MAZITO MWIGULU KUTUMBULIWA…!', 'GHAFLA MKE WA MAGUFULI AFA…!', 'ITAKUTOA MACHOZI UKWELI WOTE KIFO CHA MAGUFULI'.

Pia, amesema Polisi imemkamata, Joseph Mzava (19), mkazi wa Kinondoni, Dar es Salaam, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza Chuo cha Biachara Dar es Salaam (CBE), kwa tuhuma za kujinasabisha kuwa yeye ni Rais Mstaafu Jakaya Kikwete na  kufanikiwa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kupitia mtandao kwa kutumia laini za simu zenye usajili usio na majina yake.

Jeshi la Polisi pia limemkamata LI NAIYONG (48) raia wa China, ambaye anatuhumiwa kujihusisha na shughuli za kuingilia mfumo wa mawasiliano kinyume na taratibu za nchi, na kuisababishia Serikali hasara ya kiasi cha Shilingi Milioni 221,163,600.

Mtuhumiwa huyo amekuwa akituma vifaa visivyo rasmi kuwaunganisha watu kwa simu kufanya mawasiliano nje ya nchi kinyume na sheria za mamlaka ya mawasiliano Tanzania.

 Watuhumiwa hao wamekutwa wakiwa na vifaa mbalimbali ambavyo wanavitumia kufanya uhalifu huo, vifaa hivyo ni Simu za mkononi 23, laini za Simu 437 za makampuni mbalimbali ya huduma za simu zenye usajili wa watu tofauti tofauti, Kompyuta Mpakato 6, Sim Box 5, Routers 3, Power Bank.

Aidha, Jeshi la Polisi linatoa rai kwa Wananchi kuwa makini na matumizi ya mitandao ya kijamii, pamoja na kuzingatia maadili ya taaluma ya habari na sheria zinazohusika kuepuka kuchapisha taarifa  za uongo na zile zitakazo zua taharuki kwa umma.

Jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua kali kwa mtu/watu wote watakao vunja sheria, kanuni na miongozo inayoelekeza matumizi sahihi ya mitandao.