MIGODI YA BARRICK YAWEKA REKODI YA UZALISHAJI NA KUPATA THAMANI YA MUDA MREFU

Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation, Mark Bristow, akikagua Hospitali ya Bugalama, wilayani Msalala Mkoani wa Shinyanga, ambayo inasaidiwa na Mgodi wa Bulyanhulu. Kulia ni Mganga Mfawidhi wa wa hospitali hiyo, Silas Kayanda. Wengine ni Maofisa  wa Serikali na wafanyakazi wa Barrick Bulyanhulu.

Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation, Mark Bristow,akiongea katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya kampuni uliofanyika katika mgodi wa Bulyanhulu. Kushoto ni Naibu Waziri wa Madini, Dk.Steven Kiruswa na kulia ni Meneja wa Barrick Tanzania-(Utawala na Fedha), Melkiory Ngido.

Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation, Mark Bristow, akikabidhi mfano wa hundi ya dola 10,000 za Kimarekani kwa Mwakilishi wa Asasi isiyo ya kiserikali ya Hope for Girls and Women Tanzania, Rhobi Samwelly, kusaidia shughuli za asasi hiyo, mkoani Shinyanga. Kulia ni Naibu Waziri wa Madini, Dk. Steven Kiruswa.

Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Barrick Cooperation, Mark Bristow akikabidhi mfano wa hundi ya dola 10,000 za Kimarekani  kwa kinamama wa Kikundi cha Wanawake waponda kokoto cha Bugalama, Martha Mgeta (wa pili kushoto) na Naomi Christopher, mkoani Shinyanga. Kulia ni Naibu Waziri wa Madini, Dk. Steven Kiruswa.

 

NA MWANDISHI WETU

Kampuni ya Dhahabu ya Barrick  inayomiliki mgodi wa North Mara na Bulyanhulu, imeongeza pato lake hadi kufikia wakia 547,000 kwa mwaka 2022, na kufanikisha kuelekea katika hadhi ya Daraja la Kwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari, juzi, Rais na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Barrick, Mark Bristow, alisema tangu kampuni ichukue jukumu la udhibiti wa migodi hiyo mwaka 2019 imefanikiwa kufanya mageuzi makubwa katika shughuli zilizokuwa zimekufa.

Bristow alisema utafutaji wa madini unaendelea kutoa fursa za kuongeza ukubwa wa akiba ya miamba yenye madini katika migodi yote miwili.

Alisema kipindi cha mpito cha mgodi wa North Mara kuelekea uchimbaji wa mmiliki unafanikiwa kwa kuongeza kwa kasi upanuzi wake unaoendelea wa chimbo la wazi kukiwa na uboreshaji wa ufanisi na gharama, wakati maendeleo ya kiteknolojia katika shughuli za uchimbaji wa chini kwa chini yanaongeza tija.

"Mwaka jana, North Mara ilitambuliwa rasmi kama mlipakodi mkubwa zaidi wa Tanzania na Bulyanhulu ilitunukiwa tuzo ya Mwajiri Bora Anazingatia Masharti na Matakwa ya Sheria, iliyotolewa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii. North Mara na Bulyanhulu pia zilipokea tuzo za mshindi wa kwanza na wa pili mtawalia za kutambua mchango wao kwa Uuzaji wa Madini nje ya nchi na kwa uzalishaji wa fedha za kigeni na Migodi yote miwili imetoka mbali sana na tunatarajia kuendelea na safari hiyo kupitia ubia wetu wa Twiga na serikali”, alisema Bristow.

Alisema tangu ichukue jukumu la udhibiti mnamo mwaka 2019, Barrick imeingiza dola za kimarekani bilioni 2.4 katika uchumi wa Tanzania. Mwaka jana, ililipa dola za kimarekani milioni 303 za kodi, mrabaha, ushuru, gawio na ulipaji wa mikopo ya wanahisa na dola za kimarekani milioni 476 kwa wasambazaji na watoaji wa huduma wa ndani .

Bristow alisema kadiri migodi ilivyoendelea kukua, imeendelea kuweka kipaumbele cha utoaji wa ajira kwa watu wa ndani na Watanzania 96%, huku 45% ya waajiriwa wapya wakitoka katika jamii zinazoizunguka migodi hiyo.

Pia alisema kupitia kamati za maendeleo ya jamii, migodi hiyo imewekeza zaidi ya dola za kimarekani milioni 10 katika miradi ya kuboresha huduma za afya, elimu, upatikanaji wa maji ya bomba na miundombinu ya barabara.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madin Dkt. Steven Kiruswa, ameishukuru Barrick na Kampuni tanzu ya Twiga kwa mafanikio makubwa yanayozidi kuonekana kupitia uwekezaji hapa nchini.

“Tuendelee kupiga vita utoroshaji madini, tuendelee kuwapa ushirikiano kampuni ya Barrick ili uwekezaji uwe na tija kwa wananchi. Tunataka kampuni ziwape kipaumbele wazawa ambapo tunashukuru Barrick imeajiri watanzania asilimia 96%”. alisema Dk. Kiruswa.

Kwa upande wa Mbunge wa Msalala, Idd Kassim, alisema uhusiano uliopo kati ya Mgodi wa Bulyanhulu na jamii ni mzuri ambapo fedha zinazotolewa na mgodi zinaleta tija kwa jamii.