RPC ILALA AWATAKA WAZAZI KUWALINDA NA KUWASIMAMIA WATOTO WAO KATIKA MALEZI KUWAEPUSHA NA UKATILI WA KIJINSIA






 

NA MWANDISHI WETU

Kamanda Polisi Mkoa wa Ilala, Debora Magiligimba, amewataka wazazi kusimamia malezi ya watoto wao kuepuka vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Dabora alitoa wito huo, wakati wakifanya usafi katika Soko la Samaki la Kimataifa Feri, Kata ya Kivukoni, Dar es Salaam, jana.

Alisema wazazi wanapotoka kwenda katika shughuli zao waache watoto katika mazingira salama ikiwemo hata kuwapeleka kwa jirani ambako kutakuwa na watu wazima wa kuwaangalia.

"Wazazi wenzangu tuwalinde watoto wetu kama sisi tulivyolindwa, tusiwaache peke yao dunia ya sasa siyo ile ya zamani, tunaporudi katika kazi zetu tutafute muda wa kukaa na kuwakagua watoto wetu", alisema.

Debora alisema wazazi wazungumze na watoto kuwauliza kuhusu changamoto wanazokutana nazo sheleni, kuna baadhi ya watoto wanabakwa hadi wanapona na wazazi hawajui, hivyo wazazi wabadilike na walinde watoto.

Kwa upande wa wake, Mkuu wa Daawti la Jinsia na Watoto Mkoa wa Kipolisi Ilala, Dk. Christina Onyango, alisema vitendo vya ukatili wa kijinsia ni kumfanyia mtu kinyume na matakwa yake.

Alisema ndani ya Jeshi la Polisi kuna kitengo cha dawati la kijinsia na watoto, ambacho kinashughulikia kesi zote za ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.

Dk. Christina alisema hata wanaume wanapofanyiwa ukatili wa kijinsia na wake zao kwa kupigwa au kuchomwa moto  wasiogope kutoa taarifa katika dawati hilo.

"Wakina baba mkiona mnapigwa unatakiwa mje kutoa taarifa katika dawati letu la kijinsia na watoto, kama vile kuchomwa moto, kunyimwa unyumba, ukiona kila siku hadi mwezi mzima ikifikia hivyo njoo utoe taarifa katika dawati letu", alisema.

Pia Dk. Christina alisema pia lugha za matusi ni ukatili wa kijinsia ikiwemo kuwaita watoto wetu majina ya wanyama, kutoleana siri katika tendo la ngono na kuna baadhi wanajirekodi wakikorofishana wanavujisha picha zao katika mitandao ya kijamii.

Naye Meneja wa Soko hilo, Denis Mrema, imeliongeza Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na jamii, ikemo kufanya usafi katika soko hilo.

Mrema alisema kitendo walichofanya jeshi la polisi ni kuleta ushirikiano wa wananchi na jeshi hilo, pia itasaidia kufichua wahalifu.