AFYA YA MAJERUHI WA AJALI YA MWENDOKASI YAZIDI KUIMARIKA-MOI

Meneja uhusiano wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), Patrick Mvungi (kushoto), akiwa na ndugu wa Osam Milanzi, pamoja na mke wake, Isha Mohamed (katikati), baada ya kumtambua majeruhi huyo wa ajali ya Mwendokasi, iliyokea hivi karibuni.

 

NA MWANDISHI WETU

Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), imesema afya ya Osam Milanzi, ambaye ni majeruhi wa ajali ya mwendokasi, imeimarika kutokana na kazi kubwa inayofanywa na madaktari, wauguzi na watumishi wengine wa MOI.

Akitoa taarifa kwa umma, Meneja uhusiano wa MOI Patrick Mvungi, amesema Milanzi ametambulika kwa jina lake ni Osam Milanzi, mkazi wa Manzese Midizini.

Mvungi amesema utambuzi umefanywa na mke wake, Isha Mohamed na mdogo wa Osam, anayeitwa, Shaban Milanzi. 

Pia Mvungi ametoa shukrani kwa vyombo vya habari na Watanzania wote walioshirikiana taasisi hiyo kutangaza habari za kuwatafuta ndugu Milanzi na hatimaye kupatikana.

Kwa upande wa mdogo wa Milanzi, Shaban Milanzi, ameshukuru Madaktari kutokana na jitihada kubwa za kumtibu ndugu yao mpaka hivi sasa anaendelea vizuri.

"Kwa kweli namna tulivyoiona hiyo ajali kupitia mitandao ya kijamii, hatukudhani kama tunaweza kumkututa ndugu yetu, lakini yupo anaendelea kutibiwa na hali yake inaendelea vizuri’’, amesema.

Shabani amesema amemuona na kuthibitisha ni ndugu yao na kweli ameumia ila wanamshukuru Mungu kwa sababu anaendelea kupata matibabu, na kwamba tunawashukuru Madaktari kwa sababu nanma wanavyopambana naye utafikiri ni mtu wanaye mjua. 

Ajali hiyo ya basi la mwendokasi ilitokea Februari 22, 2023 saa 12 asubuhi, katika eneo la kisutu baada ya kugongana na gari dogo na kusababisha kugonga jengo lililokuwa jirani ambapo Osam alikuwa akitembea kwa miguu.