MBELGIJI ADEL AMROUCHE, KOCHA MPYA WA TAIFA STARS

Kocha mpya wa  Taifa Stars, Mbelgiji Adel Amrouche

NA MWANDISHI WETU

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imemtangaza, Adel Amrouche, kuwa kocha mpya wa timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars'.

Kocha Amrouche ni raia wa Ubelgiji, mwenye asili ya Algeria, ni mzoefu wa soka la Afrika, kufuatia kufundisha klabu na timu za taifa katika nchi za Kusini, Mashariki, Kati na Kaskazini.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari,  Ofisa Habari wa TFF, Cliford Ndimbo, amesema kocha  Amrouche amewahi kuwa kocha bora wa Afrika Mashariki mwaka 2013, wakati akiifundisha na kuipa ubingwa wa michuano ya Kombe la Chalenji, linaloandaliwa na Baraza la Vyama Vya Soka Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Challenge).

Kocha huyo aliipa mafanikio timu ya Kenya ‘Harambee Stars’, akiwa na kikosi hicho aliweka rekodi ya kucheza michezo 20 bila kupoteza na kuifikisha nusu fainali mara mbili akiwa Burundi", amesema.

Ndimbo amesema kocha huyo aliwahi kuzinoa timu za taifa za Equatorial Guinea, Botswana, Libya na Yemen kwa wakati tofauti.

Amesema wakati anainoa DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo,  aliiwezesha kufanya vizuri katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika na kuipa mara mbili ubingwa wa nchi hiyo na michuano ya DRC Super Cup.

Pia Ndimbo amesema kocha huyo ana uzoefu wa klabu, alishazifundisha timu za RC Kouba, USM Alger, MC Algires zote za Algeria ambapo aliwahi kuzichezea.

Ofisa huyo wa TFF, amesema Kocha Amrouche ni mkufunzi wa walimu wa leseni ya Pro wa Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) na amezalisha makocha wengi bora Afrika huku akiwa na uzoefu wa soka la vijana, kazi aliyoifanya kwa kipindi cha miaka 10 nchini Algeria na Ubelgiji.

 
Amesema Kocha Amrouche ana wezo wa kuzungumza lugha za Kiswahili, Kiarabu, Kiingereza na Kifaransa na amewahi kuwa Mkurugenzi wa Ufundi na Michezo katika klabu za Ubelgiji na Ukraine.

Kocha huyo ana leseni ya Pro nashahada ya uzamili, katika kuwasoma watu na utimamu, amekuwa akifanya kazi ya ukufunzi pia katika Shirikisho la Soka Afrika (CAF) katika kuzalisha makocha wa soka ambapo kwa kipindi chote cha mkataba wake atakuwa akilipwa mshahara na serikali.