MJUMBE WA KAMATI KUU YA CCM TAIFA, SPIKA DKT. TULIA: CCM HAITOACHIA DOLA KAMWE, HATUNA MPANGO WA KUMPISHA MTU





 

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Mhe. Dkt. Tulia Ackson amesema kuwa hakuna siku itatokea chama hicho kikaruhusu nafasi ya kuachia kuitawala nchi kwakuwa imejiwekea mizizi imara katika kuwatumikia wananchi wake.

Dkt. Tulia ameyasema hayo leo Februari 4, 2023 akiwa Visiwani Zanzibar kwa ziara ya kichama ambapo alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya sherehe za miaka 46 ya Chama hicho iliyofanyika katika Mkoa wa kusini Unguja.

Amesema kuwa ni wakati sahihi kwa wanachama wa chama hicho hususani vijana kuendelea kukipigania na kuwapigania Viongozi wao wakuu akiwemo Mwenyekiti wa Chama taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuyasemea mazuri anayoyafanya kwa nchi.

“Mwana CCM hupaswi kukaa kinyonge hata siku moja, kote Tanzania bara na visiwani kuna miradi ya ujenzi wa shule kila kona, miundombinu ya barabara, zahanati, vituo vya afya n.k haya yote ni mafanikio ya kujivunia sasa unakaaje kinyonge? tunaposema kwamba chama hiki hakitaachia dola tunamaanisha” Amesisitiza Dkt. Tulia