SERIKALI YAIPONGEZA MGODI WA DHAHABU WA BARRICK BULYANHKULU KWA KUTEKELEZA MIRADI YA MAENDELEO KWA WANANCHI

Mkuu wa Shule ya Sekondari  Mwingiro, wilayani Msalala, Mkoa wa  Shinyanga, Antony Fabian (Katikati),  akitoa maelezo kuhusu ujenzi wa madarasa kwa ujumbe kutoka Ofisi ya Rais  Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),  ukiongozwa na Mkurugenzi wa sera na Mpango kutoka (TAMISEMI), John Cheyo (mwenye kofia),  wakati wakikagua miradi mbalimbali iliyotekelezwa fedha za uwajibikaji kwa jamii (CSR)  zilizotolewa na Mgodi wa Barrick Bulyanhulu,  mwishoni mwa wiki, mkoani humo.

Mkurugenzi wa Sera na Mpango Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa a Serikali za Mitaa (TAMISEMI), John Cheyo  (mwenye kofia),  akikagua Kituo cha Afya  Bugarama, wakati  wa ziara ya kukagua miradi mbalimbali iliyotekelezwa kwa fedha za uwajibikaji kwa jamii (CSR)  zilizotolewa na Mgodi wa Barrick Bulyanhulu,  mwishoni mwa wiki.

 

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI imeipongeza Mgodi wa dhahabu wa Barrick Bulyanhulu, mkoani Shinyanga, kwa kutekeleza miradi ya kijamii na kuboresha maisha ya wananchi kwa kupitia fedha za uwajibikaji kwa jamii (CSR). 

Pongezi hizo zimetolewa na Mkurugenzi wa Sera na Mipango-Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),  John Cheyo, wakati maofisa wa TAMISEMI wakikagua miradi ya afya na elimu iliyotekelezwa kupitia fedha za uwajibikaji kwa jamii (CSR).

Miradi hiyo imetekelezwa kutoka na fedha hizo zilizotolewa na mgodi wa Barrick Bulyanhulu katika Halmashauri za Wilaya ya Msalala na Nyang’hwale katika Mikoa ya Shinyanga na Geita.

Cheyo, amesema amefurahishwa kukamilika kwa miradi hiyo  mbalimbali katika sekta ya elimu na afya ambayo miundombinu  yake imejengwa kwa viwango vya kuridhisha kwa kutoa huduma bora kwa wananchi na kuchochea kufanikisha mipango ya Serikali ya kuleta maendeleo kwa wananchi hususani katika sekta ya elimu na afya.

“Nawapongeza Barrick Bulyanhulu na Watendaji wa Serikali kwa kusimamia ujenzi wa miradi hii na natoa wito kwa watumiaji wa majengo na vifaa vilivyonunuliwa mahospitalini kuvitunza na kuendelea kuhudumia wananchi wengi zaidi katika kipindi cha muda mrefu", alisema.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Mahusiano ya Jamii na Mazingira wa Barrick Bulyanhulu, Zuwena Senkondo, amesema miradi ikishapitishwa na halmashauri husika, mgodi unatoa fedha zilizotengwa kwa kufanikisha mradi hiyo, wanafanya ufuatiliaji kuhakikisha inatekelezwa kwa viwango na  muda uliopangwa.

Zuwena amesema miradi iliyotekelezwa kwa fedha za CSR za kutoka mgodi huo ni  Shule ya Sekondari ya Mwingiro, Shule ya mchepuo wa Kingereza ya Kharumwa, ujenzi wa madarasa na kuboresha maabara katika Shule za Sekondari za Kayenze, Igalula, Busulwangili, Bugarama, Chuo cha VETA Bugarama, Chuo cha Wauguzi cha Ntobo na Kituo cha Afya cha Bugarama.

Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari  Mwingiro, Antony Fabian, ameishukuru serikali na Mgodi wa  Barrick Bulyanhulu, kwa kutekeleza miradi hiyo.

Amesema miradi hiyo mikubwa itasaidia kuboresha sekata ya elimu na afya na kuboresha maisha ya wananchi.