NA MWANDISHI WETU
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas, amesema mashindano ya majeshi ambayo yalikuwa yanafanyika yameongeza kipato katika mkoa wake.
Mashindano hayo ambayo yaliandaliwa na Baraza la Michezo ya Majeshi
Tanzania (BAMMATA), yalifanyika kwa siku 14 katika viwanja vya Chuo cha Ufundi
na Nangwanda.
Timu zilizokuwa zinashiriki mashindano hayo ni Uhamiaji, SMZ,
Magereza, Polisi, JKT, Ngome na Zimamoto zikicheza michezo ya riadha, mpira wa
miguu, mpira wa kikapu, mpira wa mikono, mpira wa wavu, netiboli, ngumi, judo
na kurusha shabaha.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Kanali Abbas, kulikuwa na
idadi ya watu wasiopungua 5000 waliokuwa wanashiriki mashindano haya.
“Watu wamekula, wamekunywa na kulala hii kwetu imeongeza pato la
mkoa naamini hata wafanyabiashara walikuwa na furaha wakati mwingi,”
amesema.
Alisema mashindano hayo pia yameongeza uhusiano mzuri kati ya vyombo
vya ulinzi na wakazi wa mkoa huo kutokana na kuwa nao kwa karibu.
“Jeshi na wananchini ni watu tunaoshirikiana vizuri, kama mlivyoona
wamejitokeza kuchangia damu ambazo zitawasaidia wagonjwa wa mkoa wangu hii
kwetu ni kubwa sana,”amesema.
Mashindano yalianza kutimua vumbi Februari 9 hadi Februali 21na
yalifungwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini.