BARRICK NORTH MARA NA WAKANDARASI WAKE WATOA MSAADA WA VIFAA TIBA KWA KITUO CHA AFYA WILAYANI TARIME

Meneja Mkuu wa mgodi wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko (Kulia) akisalimiana na Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara, wakati wa kukabidhi msaada wa vifaa tiba katika kituo cha afya cha Sungusungu kilichopo Nyamongo wilayani Tarime, uliotolewa na kampuni hiyo kwa kushirikiana na wakandarasi wake.
Meneja Mkuu wa mgodi wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko (Kulia)  na Mbunge wa Tarime Vijijini Mwita Waitara (katikati),  wakikata utepe wakati wa kukabidhi msaada wa vifaa tiba katika kituo cha afya cha Sungusungu kilichopo Nyamongo wilayani Tarime, uliotolewa na kampuni hiyo kwa kushirikiana na wakandarasi wake, wilayani Tarime.


Na Mwandishi Wetu

Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara na wakandarasi wake, wameunga mkono juhudi za serikali  katika sekta ya afya kwa kutoa  msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 120 katika Kituo cha Afya Sungusungu kilichopo Nyamongo wilayani Tarime.

Msaada huo ulikabidhiwa, jana katika kituo hicho, ambapo Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick North, Apolinary Lyambiko, alisema wameshirikiana na  wakandarasi wake kuchanga  Dola 59,587.60 kwa ununuzi na ufungaji wa vifaa hivyo.

Lyambiko alisema vifaa hivyo vilivyokabidhiwa vitasaidia kuwezesha upatikanaji wa huduma bora za afya zikiwemo za mama na mtoto katika kituo hicho, na kwamba msaada huo ni sehemu ya uwajibikaji wa mgodi wa North Mara na wakandarasi hao kwa jamii inayouzunguka.

"Desemba mwaka jana mimi na wafanyakazi wenzangu tulikagua kituo hiki na kujionea mapungufu ya vifaa tiba. Kwa kuzingatia umuhimu wa kituo hiki katika utoaji wa huduma za afya kwa wananchi na wafanyakazi wa mgodi, Januari 2023 niliagiza idara yetu ya Mahusiano na ile ya Afya kuandaa kikao na wakandarasi wanaofanya kazi mgodini ili kwa pamoja tuone namna tunavyoweza kuchangia manunuzi wa vifaa tiba,” alisema.

Alisema malengo ya mgodi ni kuendelea kushirikiana na wakandarasi wote kama wadau muhimu katika kutekeleza shughuli mbalimbali za uwajibikaji kwa jamii inayowazunguka  kuimarisha mahusiano na mshikamano.

Lyambiko alisema kampuni za wakandarasi zilizoshirikiana na mgodi huo kufanikisha msaada ni  Kemanyanki, RES, Wings, Boart Longyear, AKO  na PKM.

Kwa upande wa Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara,  aliwashukuru mgodi wa North Mara na wakandarasi hao, kwa kusema wameweka alama nzuri katika eneo hilo.

“Haya yote ni matunda ya mahusiano na ushirikishwaji na nawahidi kuwa nitawaandikia  barua ya kuushukuru Mgodi na wakandarasi hao kutokana na msaada huo wa vifaa tiba.

Pia Waitara amewaomba wadau hao wa maendeleo kuangalia uwezekano kutoa msaada wa ujenzi wa majengo ya huduma za upasuaji na za mama na mtoto katika kituo hicho.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Sylvanus Gwiboha, alisema masaada huo una maana kubwa katika utoaji wa huduma bora za afya.

 "Afya bora haiwezi kupatikana kama hakuna vifaa tiba bora. Ninaamini Mungu atawabariki kwa kazi hii nzuri. Vifaa mlivyotoa vitawapunguzia wananchi gharama za kusafiri kwenda wilayani kutafuta huduma za vipimo vya afya", alisema Gwiboha.

Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Wilaya ya Tarime, Malema Soro,  amewataka viongozi wa ngazi mbalimbali kuhakikisha mgodi wa North Mara na wadau wote wa maendeleo katika eneo hilo hawabughudhiwi katika utekelezaji wa shughuli zao.

“Viongozi tusimamie wadau hawa wasibughudhiwe katika kazi zao maana wakizalisha zaidi watatoa kitu kikubwa zaidi kwa jamii. Hapa wamemsaidia Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kutupatia vifaa tiba ambavyo vinakwenda kusaidia wananchi wetu,” amesema Malema.

 Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.