DUWASA IMEOKOA SH. BILIONI 1.121 UTEKELEZAJI WA MRADI WA MAJI, CHAMWINO







Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amezindua mradi wa tenki la kuhifadhia maji la ujazo wa lita milioni 2.5 eneo la Buigiri, wilayani Chamwino, ambao umegharimu zaidi ya sh. bilioni moja,  kuelekea maadhimisho ya siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Aprili 26.

Aidha, ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) kwa kuokoa asilimia 50 ya kiasi cha sh. bilioni 2.5 kilichotolewa na serikali kwa utekelezaji wa mradi huo.

Akizungumza baada ya uzinduzi huo,  Senyamule, amesema mradi huo ulitakiwa kutumia sh bilioni 2.5 hadi kukamilika kwake kama ungetekelezwa na Mkandarasi, DUWASA iliamua kutumia force account.

“Mradi huu utaongeza upatikanaji wa maji katika Wilaya ya Chamwino kutoka asilimia 42 mpaka asilimia 87 hivyo zaidi ya asilimia 50 yaliyokuwa yanapatikana yanaenda kupatikana Mji wa Chamwino” amesema  Senyamule.

Pia amewapongeza DUWASA kwa sababu wametumia shilingi bilioni 1.121 badala ya shilingi bilioni 2.5 hivyo wameokoa asilimia 50 ya fedha iliyotolewa na serikali kutekeleza mradi huo.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba, amesema katika kukabiliana na changamoto ya maji Dodoma wizara inaendelea kuimarisha huduma kwa kutekeleza miradi mbalimbali.

Amesema uchimbaji wa visima pembezoni mwa miji ambapo hivi karibuni DUWASA wamechimba visima vitano vyenye kuzalisha maji lita milioni 7.6 kwa siku.

“Mradi huu utausisha ujenzi wa miundombinu ili kuyafikisha maji hayo kwa haraka kwa wakazi wapatao 37000 wa eneo la Nzuguni, Ilazo, Swaswa na Kisasa”, Amesema.

“Mradi huu utagharimu shiligi bilioni 4.8 na kazi inaendelea, mradi utaongeza uzalishaji kutoka lita milioni 68.7 mpaka lita milioni 76.3 kwa siku”. Amesema Mhandisi Kemikimba.

Amesema Wizara ya maji haijalala hivyo wanafanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha maeneo mengi yanafikiwa na huduma ya maji hii ni pamoja na kuchimba visima maeneo ya Zuzu na Fufu ili tatizo la maji linapungua.

Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais, Abdallah Hassan Mitawi, amesema wanapozindua miradi mbalimbali ya maendeleo ni kielelezo cha kuonyesha kwamba kuna mambo makubwa yamefanyika katika Nyanja za kijamii, kisiasa na uchumi na ndio maana leo wananzindua mradi wa maji.

Kwa upande wa Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya DUWASA, Profesa Davis Mwamfupe, DUWASA na Wizara imekuwa ikiunga mkono kwa vitendo juhudi ya serikali kuhamisha makao makuu ya serikali kuja Dododma na kuwaomba wanufaika wa mradi huo kutumia vizuri ili yatakayobaki yasaidia maeneo yenye uhaba.

Awali akitoa taarifa ya mradi, Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph amesema mahitaji ya maji kwa sasa katika mji wa Chamwino ni wastani wa lita milioni 3.6 kwa siku na kinachozalishwa ni lita milioni 4.9 kwa siku hivyo kuwa na ziada uzalishaji.

Mhandisi Aron ameeleza kuwa huduma ya maji inayotolewa kupitia visima vinne vinavyofanya kazi kwa sasa ni kuhudumia wananchi kwa asilimia 87 katika eneo hilo kulingana na mtandao ambao tayari umetengenezwa.