BARRICK NA SHIRIKA LA NVeP WACHANGIA DOLA 10,000 KATIKA SHULE YA WENYE MAHITAJI MAALUMU SHINYANGA

Na Mwandishi Wetu

KATIKA kuunga mkono juhudi za serikali za kuboresha sekta ya elimu, Shirika la ya Nos Vies en Partage Foundation (NVeP) na  Kampuni ya Barrick, wametoa msaada wa dola za kimarekani 10,000 kwa Shule ya Msingi ya watoto wenye mahitaji maalumu Buhangija, mkoani Shinyanga. 

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi msaada huo,  mwishoni mwa wiki, katika Mgodi wa Bulyanhulu, wilayani Msalala,  Meneja Mkuu wa Mgodi huo, Cheick Sangare, alisema kila robo ya mwaka, taasisi hiyo imetoa misaada yenye tija na manufaa ya moja  kwa  moja kwa jamii zenye uhitaji.

Alisema hadi sasa wametoa msaada kwa zaidi ya mashirika 10 nchini Tanzania kupitia taasisi ya NVeP, na sasa wanaleta  mabadiliko kwa Shule ya Msingi Buhangija ambayo inatoa elimu kwa watoto wenye mahitaji maalum kwa kuipatia  msaada wa dola za kimarekani 10, kwa ajili ya kuboresha mazingira ya wanafunzi kupata elimu.

Pia alisema msaada huo umetokana na sehemu ya fedha zilizotolewa na taasisi ya Nos Vies en Partage (NVeP), iliyoanzishwa na inayofadhiliwa na Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Barrick Gold Corporation, Mark Bristow, kwa kusaidia makundi maalumu yakiwemo  Wanawake, watoto na makundi mengine yenye uhitaji yasiofaidika na ukuaji wa kiuchumi barani Afrika.

Kwa upande wake  Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Fatuma Gilalah,  ameishukuru kampuni hiyo na shirika hilo kwa msaada huo ambao utasaidia kutatua changamoto mbalimbali kwa kuboresha mazingira ya wanafunzi wake.

Alisema jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali kuboresha mazingira ya kuwapatia elimu watoto wenye mahitaji maalumu wanaosoma katika shule  hiyo bado kuna changamoto mbalimbali kwa upande wa miondombinu na vifaa vya kufundishia.

“Tunashukuru kwa msaada huu tuliopokea siku ya leo kutoka Barrick na  utasaidia kuboresha mazingira  ya kusomea ya wanafunzi wetu," alisema Gilalah.

Alisema shule hiyo inatoa elimu kwa wanafunzi wenye ulemevu wa ngozi (albino),wasioona na wenye usikivu hafifu vizuri.

MENEJA Mkuu wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Cheick Sangare (wa pili kulia), akimkabidhi  Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya watoto wenye mahitaji maalumu Buhangija, Fatuma Galalah (katikati), msaada wa mfano wa hundi ya dola 10,000,  zilizotolewa na taasisi ya Nos Vies en Partage (NVeP),  inayofadhiliwa na Rais na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation, Mark Bristow, mkoani Shinyanga, mwishoni mwa wiki.

MENEJA Mkuu wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Cheick Sangare (wa pili kulia), akimkabidhi Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Buhangija ya watoto wenye mahitaji maalumu, Fatuma Gilalah (katikati), msaada wa mfano wa hundi ya dola 10,000,  zilizotolewa na Taasisi ya Nos Vies en Partage (NVeP),  inayofadhiliwa na Rais na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation, Mark Bristow, mkoani Shinyanga, mwishoni mwa wiki.