FEDHA ZA BARRICK ZIMEINUA SEKTA YA AFYA NA ELIMU SHINYANGA NA GEITA

 NA MWANDISHI WETU

 Fedha za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) zilizotolewa na Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, zimejenga zaidi ya zahanati 15 na kuboresha miundombinu barabara na shule katika Halmashauri  ya Wilaya ya Nyang’hwale, mkoani mkoani Geita.

Ofisa Mwandamizi wa Mahusiano ya Jamii na Usimamizi wa miradi Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Zuwena Senkondo, alisema hayo juzi, wakati Wajumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC) wakiongozwa na Kaimu Katibu Tawala wa mkoa wa Mara, Dominicus Lusajo, walipotembelea na kujifunza mgodi huo ulivyotekeleza miradi ufanisi.

Zuwena amesema katika kipindi cha 2022 na 2023 Barrick Bulyanhulu kupitia fedha hizo imfanikiwa kuboresha maisha ya Wananchi na kufanya maeneo yenye miradi hiyo kuvutia zaidi katika katika wilaya za Kahama, Nyang’hwale na Msalala.

Amesema miradi iliyojengwa kupitia fedha za CSR za Barrick Bulyanhulu ni Chuo cha Ufundi Stadi cha Bugarama, Hospitali ya Bugarama, Shule ya Wasichana ya Bulyanhulu.

Pia fedha hizo zimejenga Chuo cha Mafunzo ya Afya cha Ntobo, Kituo cha mabasi cha Segese, Shule ya awali na msingi ya mchepuo wa Kingereza ya Kharumwa pamoja na miradi ya maji safi na  barabara.

Kwa upande wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Dominicus Lusajo, ameipongeza  kampuni ya Barrick kwa kufanikisha miradi ya maendeleo hususani katika maeneo yanayozunguka  migodi yake ya Bulyanhulu na North Mara.

Amesema ziara  hiyo wataweza kujifunza jinsi ya kuibua na kutekeleza miradi yenye tija na kuisimamia kwa ufasaha.

Naye Mbunge wa Tarime vijijini, Mwita Waitara, amesema kampuni hiyo imekuwa ikitekeleza vitendo sera za Serikali kuhusu uwekezaji katika sekta ya madini.

Waitara amesema wananchi wanaoishi jirani na migodi hiyo wameanza kufaidi matunda ya uwekezaji huo kupitia miradi mbalimbali iliyoanzishwa, kupata zabuni za kutoa huduma migodini na ajira kwa wananchi kutoka maeneo hayo na watanzania wote kwa ujumla.

 OFISA Mwandamizi wa Mahusiano ya Jamii na Usimamizi wa miradi  Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Zuwena Senkondo, akizungumza na wajumbe  wa  Kamati ya Maendeleo ya Mkoa wa Mara, wakati wa ziara ya mafunzo na kukagua miradi iliyotekelezwa kwa fedha za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) zilizotolewa na Mgodi wa Barrick Bulyanhulu katika mikoa ya Shinyanga na Geita. (Na Mpigapicha Wetu).

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Dominicus Lusajo, akizungumza na wajumbe  wa  Kamati ya Maendeleo ya Mkoa wa Mara wakati wa ziara ya mafunzo na kukagua miradi iliyotekelezwa kwa fedha za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) zilizotolewa na Mgodi wa Barrick Bulyanhulu katika Mikoa ya Shinyanga na Geita. (Na Mpigapicha Wetu).