POLISI KUPATIWA MAFUNZO KOREA

Askari Polisi kutoka Jeshi la Polisi Tanzania wanatarajia kupata mafunzo nchini Korea, ikiwa ni utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano baina ya Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Serikali ya Korea (KOICA) na Jeshi la Polisi Tanzania.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Camillus Wambura, amesema hayo, wakati wa hafla ya kusaini makubalinao ya ushirikiano wa miaka mitatu wenye lengo la kushirikiana katika nyanja mbalimbali.

Wambura amesema kupitia mafunzo hayo Maofisa, Wakaguzi na Askari wa Vyeo mbalimbali watapata mafunzo nchini Korea na hapa nchini ikiwemo ya Upelelezi wa Makosa ya Kimtandao, Upelelezi wa Makosa ya Unyanyasaji na ukatili wa Kijinsia na Uchunguzi wa Kisayansi.

Amesema ushirikiano huo utawezesha pia Askari wa Tanzania kujua Askari wenzao wa Korea wanavyofanya kazi kwa kubadilishana uzoefu jambo ambalo litasaidia Jeshi la Polisi Tanzania kubadilika na kuwa la kisasa na weledi zaidi.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mkaazi wa KOICA Tanzania, Manshik Shin, amesema ushirikiano huo ni mwendelezo wa ushirikiano uliodumu kwa miaka mingi baina ya Korea Kusini na Tanzania ambapo wamekuwa wakishirikiana ambapo tangu mwaka 2002 zaidi ya Maofisa wa Serikali 2000 wamepata mafunzo ya muda mfupi na mrefu nchini Korea Kusini na nchi hiyo pia imeweza kutoa wataalamu zaidi ya 2000 ambao walijitolea  katika nyanja mbalimbali hapa nchini.

Naye Balozi wa Korea Kusini, Sunpyo Kim, amesema Jeshi la Polisi Tanzania, limekuwa likifanya vizuri katika kutekeleza majukumu yake ikiwemo kuhakikisha usalama wa Wafanyakazi na Wataalamu mbalimbali ambao wamekuwa wakijitolea katika kutekeleza majukumu yao hapa nchini.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Makamishna wa Polisi, Mwakilishi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Maofisa kutoka Ubalozi wa Korea na KOICA.