SASA WATEJA BENKI YA LETSHEGO KUTUMIA MATAWI YA TCB

 
Na Mwandishi Wetu
 
Benki ya Biashara Tanzania (TCB) na ile ya Letshego Tanzania zimekubaliana kuanza kufanya kazi kwa karibu ili ushirikiano wao wa kibiashara uwe ni wa manufaa makubwa na tija katika kusambaza huduma za kibenki kwa wateja nchini.
 
Katika kulitimiza hilo, jana benki hizo ziliingia makubaliano yanayowawezesha wateja wa Letshego kuweka pesa kwenye akaunti zao kupitia matawi ya TCB.
 
Akizungumza kabla ya utiaji saini wa makubaliano hayo jijini Dar es Salaam, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa TCB, Bw Jema Msuya, alisema fursa hiyo ya kipekee itakuwepo pia kupitia mawakala wao zaidi ya 5,000 waliotapakaa nchi nzima.
 
Kiongozi huyo alibainisha kuwa sasa wateja hao wana fursa ya kuweka amana kupitia matawi 90 ambapo 82 ni yale yanayomilikiwa na TCB na yaliyobaki yakiwa ni ya mshirika wake mpya wa kibiashara.
 
“Huduma hii mpya tunayoizindua leo ni matokeo ya mabadiliko makubwa ya kiteknolojia ambayo yamewezesha mifumo yetu kuweza kuruhusu miamala husika kufanyika tena kwa usalama mkubwa tu,” Bw Msuya alidokeza.
 
“Ni mabadiliko haya na maendeleo ya kidijitali ambayo sasa hivi yanafanya isiwe lazima kuwa na tawi kila mahali bali kutoa fursa kuwatumia waliotayari na miundombinu sehemu husika kuweza kutanua wigo wa upatikanaji wa huduma kama walivyofanya wenzetu wa Benki ya Letshego,” alifafanua.
 
Aidha, alisema wana uzoefu na utaalamu wa kutosha katika katika michakato ya aina hiyo na mipango yao ya siku za usoni kwenye ushirikiano na Letshego ni kuhakikisha pia wateja wa benki hiyo wanaweza kutoa pesa kupitia TCB.

”Sisi tupo tayari kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma za kibenki nchini kunaboreka na kuwa rahisi zaidi na tayari tumekuwa na utaratibu kama huu na wenzetu wa Benki ya Standard Chartered Tanzania,” Bw Msuya akisisitiza.
 
“Ni jambo kubwa kwetu kushirikiana na Benki ya Letshego Tanzania kuwapa wateja wao nafasi na urahisi wa kuyatumia matawi yetu na makawakala wetu kuweka fedha kwenye akaunti zao,” aliongeza na kusisitiza kuwa ushirikiano huo unaenda kuimarisha dhamira ya TCB ya  kutoa huduma bora zaidi za kibenki kwa wateja.
 
Mgeni rasmi kwenye hafla hiyo alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Letshego ambaye aliipongeza TCB kwa kukubali kusaidia kuwahudumia wateja wao akisema kitendo hicho ni cha kipekee na kihistoria kwenye tasnia ya mabenki nchini.
 
Aidha, alisema utaratibu huo mpya kwao unaendana na matarajio ya Benki Kuu ya Tanzania ya kuzisambaza huduma za kibenki kote nchini lakini pia ni mchango mkubwa katika kutekeleza ajenda ya taifa ya huduma jumuishi za kifedha.
 
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Letshego , Bw Omar Msangi, alikuwa na haya yafuatayo: “Kuanzia sasa hivi wateja wetu wanaweza kuweka fedha zao kwenye akaunti kupitia tawi lolote la TCB au mawakala wao.
 
“Kwa usalama wa hali ya juu muamala utakaofanyika utasoma kwenye akaunti zao kwetu. Ni furaha iliyoje kwetu sisi kupewa nafasi na TCB ili kuwapa njia rahisi wateja wetu kuweka fedha kwenye akaunti zao.”
 
Naye Meneja Mkuu wa Uendeshaji wa TCB, Bw Komba Tawa, aliwahakikishia huduma bora na za kisasa wateja wa Leshego akisema TCB ina uzoefu wa kutosha katika hilo kutokana  na kuwa benki kongwe kuliko zote nchini ambayo ndani ya miaka miwili ijayo itakuwa inatimiza umri wa miaka 100.

Mkurugenzi wa Tehama na Oparesheni wa Tanzania Commercial Bank (TCB), Jema Msuya (wa pili kulia) na viongozi wa benki ya Letshego,  wakishirikiana kushika bango kuzindua muungano wa benki hizo  kuweka pesa kupitia matawi pamoja na mawakala, Dar es Salaam, jana. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya Letshego, Omar Msangi,  Mwenyekiti wa Bodi ya benki hiyo, Simon Jengo na Mkuu wa kitengo cha Oparesheni, Kolimba Tawa.