MAOMBI YA FEISAL YA KUVUNJA MKATABA NA YANGA YATUPILIWA MBALI

 Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imetupilia mbali maombi ya mchezaji wa Young Africans SC, Feisal Salum la kuvunja mkataba na timu yake.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Cliford Ndimbo, amesema kamati hiyo ilisikiliza maombi hayo kwa njia ya maandishi kutoka pande zote mbili Young Africans SC na Feisal.

Amesema pande zote mbili ziliwakilishwa na wanasheria wao ambao walipewa muda nyongeza wa kufafanua walichowasilisha  katika majumuisho yao ya maandishi.

Ndimbo amesema baada kamati hiyo kupitia na kutafakari kwa kina hoja zote za pande husika, kamati imetupilia mbali maombi hayo kwa msingi kwamba ilishaamua juu ya uhalali wa mkataba wa mchezaji huyo na klabu yake ana mkataba unaendelea mpaka 2024.

Amesema kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zinazotawala uvunjaji wa mikataba ya wachezaji inayoendelea, mchezaji lazima aanze na majadiliano na klabu yake ambayo yenye haki naye.

Aidha Ndimbo amesema uamuzi kamili kwa pande zote mbili zilizokuwa zinahusika katika shauri hilo utatolewa baadaye pande husila kujulishwa.