RAIS DK. MWINYI APOKEA RIPOTI YA KAMATI YA SENSA YA WATU NA MAKAZI ILIYOFANYIKA MWAKA JANA

 Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema ina jukumu kubwa la kuzifanyia kazi Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, kujipanga na utekelezaji wa mipango ya kimaendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, aliyasema hayo Ikulu, Zanzibar, alipopokea ripoti ya Kamati ya Sensa ya Watu na makazi iliyofanyika mwaka jana.

Rais Dk. Mwinyi amesema sensa hiyo imetoa mambo mengi lazima yafanyiwe kazi kabla ya kukamilika mpango wa maendeleo 2025-2050 kuelekea mwisho wa dira ya maendeleo ambako mwaka 2030 alieleza Zanzibar inakadiriwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya watu.

Amesema ripoti hiyo na nyingine zitakazofuata lazima zitafutiwe namna nzuri ya kufanyiwa kazi kwa undani ili serikali ijipange katika masuala mazima ya maendeleo ya nchi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah, aliwaahidi Rais wa Zanzibar na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kamati yao ya ushauri ya sensa Kitaifa, itajitahidi sehemu ndogo kulikamilisha kwa vitendo zoezi hilo.

Aidha Makamu wa Pili wa Rais ambaye ni Mwenyekiti Mwenza wa Kamati hiyo amewashukuru Dk. Mwinyi na Rais Samia kwa kuiamini kamati hiyo.

Kamati ya ushauri wa sensa Kitaifa ilipewa jukumu la kuratibu na kusimamia zoezi la sensa ya Watu na Makazi Kitaifa ya mwaka 2022.