MTEMVU ATAKA KASI UTEKELEZAJI UJENZI WA SHULE ZA GHOROFA


 Na Mwandishi Wetu

 Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi  (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, Abas Mtemvu,  amepongeza utekelezaji wa Ilani  ya Chama katika Kata ya Kurasini huku akiitaka  Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kuongeza kasi katika utekelezaji wa ujenzi wa shule za ghorofa.

Amesema hayo Dar es Salaam, alipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani  ya Uchaguzi ya CCM  ya mwaka 2020/25 katika Kata ya Kurasini.

Mtemvu, ameeleza  kumekuwa na kasi ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Kata ya Kuranisi na kumpongeza Diwani wa kata hiyo Anold Peter na Chama  kwa usimamizi  wa  utekelezaji wa Ilani.

Akiwa katika Shule ya Sekondari Uhamiaji, Mtemvu, amesema yapo maelekezo ambayo yalitolewa tangu  serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Dk. Jakaya Kikwete  hajatekekelezwa.

“Kuna madarasa ya zamani  ambayo yalifanyiwa maamuzi ya kujengwa ghorofa tangu serikali ya awamu ya nne mpaka sasa hayajatekekezwa. Tutakaa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke kujadili kuhusu suala hili,”amesema Mtemvu. 

Ameongeza, awali Temeke kulikuwa na  changamoto ya maeneo  hivyo walizungumza na Rais Dk. Kikwete kutaka shule zijengwe  kwa mfumo wa ghorofa.

“Nasikitika katika shule hii (uhamiaji) watendaji wa Temeke mpaka leo  hawajatekeleza hilo. Hii siyo haki,”alisema Mtemvu.

Ameshauri uboreshaji wa mazingira na  miundombinu, hususa vyoo, kumfanya mwanafunzi kujisikia yuko shuleni.

Akikagua ujenzi wa  Zahanati ya Kurasini, Mtemvu  alisema  maelekezo ya Rais Dk. Samia ni kata zote kuwa na vituo vya afya.

“ Mpango wa serikali ni kila kata kuwa na kituo cha afya.  Tulitarajia  hapa Kurasini kukuta kiutuo cha afya.  Japokuwa wametueleza changamoto yao ni eneo ila kwa sasa ujenzi wetu ni w mfumo wa ghorofa. Hili tutazungumza pia na Manispaa ya Temeke Kurasini wapate kituo cha afya,”amebainisha.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Temeke, Zena Mgaya , ameishukuru serikali chini ya  Rais Dk. Samia kwa  kasi utekelezaji wa miradi wilayani humo.

Awali Diwani  wa Kata ya Kurasini, Anold Peter,  amemshukuru Mwenyekiti wa CCM kwa ziara hiyo  ambayo alisema  inadhirisha wajibu wa Chama kuisimamia serikali.

Pia, amepongeza serikali  kwa utekelezaji wa miradi  kabambe  maendeleo katika kata hiyo hususan sekta za barabaa, elimu, afya, uwezeshaji wananchi kiuchumi na sekta zingine.

“Mchango  huu wa maendeo pia  ni kutoka serikali Kuu.  Sisi wananchi wa  Kurasini  ametutendea haki na  sisi tunahidi kumtendea haki   2025 utakapo wadia,”alisema Peter ambaye ni Naibu Meya wa Halmshauri ya Temeke.