NI HESHIMA KWANGU KUTEULIWA BMF - BALOZI MULAMULA

Na MWANDISHI WETU

Balozi Liberata Mulamula (Mbunge), ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Benjamini Mkapa (BMF), huku akishukuru kwa kupewa heshima hiyo kuongoza Taasisi hiyo ya kubwa ya kiongozi mashuhuri nchini.

Balozi Liberata Mulamula aliteuliwa juzi na Mlezi wa Taasisi hiyo, Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ya Zanzibar, Dk.Hussein Ali Mwinyi.

Akizungumzia uteuzi huo, Balozi Mulamula alisema anashukuru kwa kupata heshima hiyo kubwa ya kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi kubwa iliyobeba jina la kiongozi mashuhuri aliyewahi kuongoza Taifa kwa mafanikio makubwa.

"Kwangu hii ni heshima kubwa kwani Benjamini Mkapa ni mlezi wangu ambapo mimi niliingia katika ofisa wa diplomasia yeye akiwa Waziri wa Mambo ya nje, nilijifunza mengi kutoka kwake naye alituongoza vyema na kutujengea uwezo.

"Siku zote alipenda bidii ya juhudi ya kazi ya mtu binafsi sio kubebwa bebwa, hivyo alitujengea uwezo mkubwa, nafurahi na niheshima kwangu kupata nafasi hii," alisema.

Aliongeza, Benjamin Mkapa ni miongoni mwa viongozi mashuhuri nchini waliofanya kazi kubwa hususan kipindi chake cha Urais, alisaidia Taifa kuvuka katika vipindi vigumu na kuimarisha diplomasia na mataifa mbalimbali ulimwenguni.

Katika hatua nyingine, Balozi Mulamula alimshukuru mlezi wa Taasisi hiyo, Dk.Mwinyi kwa kumwamini na kumteua katika nafasi hiyo huku akiahidi kushirikiana vyema na Wajumbe  wa bodi.