KOCHA YANGA ATAKA MPACHIKA MABAO


Na Mwandishi Wetu

Kocha mpya wa klabu ya Yanga, Miguel Gamondi, ameutaka uongozi wa klabu hiyo kusajili mshambuliaji mwingine atakayeongeza kasi ya upachikaji wa mabao katika kikosi hicho msimu ujao wa 2023/24.

Gamondi raia wa Argentina, atawasilini nchini leo Ijumaa 2023, kuanza kazi ya kukinoa kikosi hicho kwa mara ya kwanza, tangu alipotangazwa kuajiriwa na klabu hiyo Juni 24, mwaka huu.

Taarifa zinaeleza kuwa kocha huyo ameuomba uongozi wa Yanga kumuongezea mshambuliaji mahiri ambaye ataongeza kasi ya kupachika mabao katika kikosi hicho, kilichofika nusu fainali ya michuano kombe la Shirikisho barani Afrika.

Yanga ina washambuliaji mbalimbali akiwemo mfumania nyavu hodari, Fiston Mayele raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Mzambia Kennedy Musonda, ambao kwa pamoja waliing’arisha timu hiyo msimu uliopita.

Wakati Musonda akiisaidia Yanga kushinda mechi mbalimbali, Mayele alimaliza msimu uliopita akiwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara (mabao 16) na Kombe la Shirikisho Afrika mabao 7.

Chanzo cha taarifa hiyo imeeleza kuwa, pamoja na ubora wa nyota hao, lakini Gamondi anahitaji straika mwingine ili kuongeza nguvu katika eneo la ufungaji.

“Kocha ametoa maelekezo mengi kwa viongozi, lakini zaidi amesisitiza kuongezewa mshambuliaji ambaye atakuja kuleta ushindani katika kikosi sio wa kukaa benchi,” kimesema chanzo hicho.

Chanzo hicho kilieleza kuwa, Muargentina huyo tayari ana majina ya wachezaji aliowapendekeza, lakini atakapowasili nchini atajadiliana na uongozi.

Akizungumzia hilo, Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, amesema klabu itaweka hadharani wachezaji ambao wameshakamilisha usajiliwa wao.

“Usajili wa mwaka huu utashtua wengi, cha kufanya mashabiki na wanachama wa Yanga wasikae mbali na mitandao yetu (ya kijamii), tunakwenda kulipua mabomu,” amesema.