RC CHALAMILA ATANGAZA KAMBI UPIMAJI AFYA NA MATIBABU BURE DAR


Na Mwandishi Wetu

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ametangaza neema kwa wakazi wa mkoa huo ya kupimwa afya na matibabu bila malipo  kwa siku 10.

Akizungumza na waandishi wa habari, Chalamila, amesema upimaji na matibabu hayo vitatolewa katika kambi maalumu   zinazofahamika kama Afya Check zitakazo fanyika katika wilaya zote tano za mkoa huo.

Amesema kampeni hiyo ya Afya Check itazinduliwa Julai 10 katika viwanja vya Zhakiem Mbagala wilayani Temeke.

"Malengo ya kampeni hii ni  kuwafikia wananchi 20,000 katika mkoa wa Dar es  Salaam,"amesema Chalamila.

Ametaja magonjwa yatakayo husika kuwa ni saratani, moyo, shinikizo la damu, Ukimwi,  chanjo  dhidi ya Uviko 19, chanjo kwa watoto chini ya miaka mitano ambao hawakupata chanjo hiyo ama hawakumaliza.

Pia  huduma za magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza pamoja na uchangiaji   damu kwa hiyari.

"Huduma zote  hizi zitatolewa bila malipo. Tutakuwa  na  madaktari bingwa kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Taasisi ya Mifupa (MOI) Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI)  Chama cha Madaktari Tanzania na madaktari bingwa na wabobezi kutoka hospitali zetu za halmashauri na mikoa,"amebainisha Chalamila.

Amesema katika Wilaya ya Temeke, kambi itafanyika Julai 10 hadi 11 katika viwanja vya Zakhem Mbagala.

"Julai 12 hadi 13 kambi itafanyika Kigamboni Mji Mwema na kuendelea  katika Wilaya ya Ubungo Julai 14 na 15 katika viwanja vya Barafu'"alibainisha Chalamila.

Ameeleza, kwa upande wa Wilaya ya Kinondoni, kambi itafanyika Julai 16 na 17 katika viwanja vya Tanganyika Packers na kuhitimishwa na Wilaya ya Ila Julai  18 na 19 katika viwanja vya Mnazi mmoja.

Awali Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Rashidi Mfaume, aliwataka wanchi kujitokeza kwa wingi kwani kambi hiyo ya Afya Check inalenga kusogeza huduma kwa jamii.

Mratibu wa Kambi hizo, Dk. Isaack Maro,  amesema alisema magonjwa yasiyo ya kuambukiza kutoka na mtindo wa maisha na aina ya chakula.

Mkurugenzi  Mtendaji wa ORCI Dk.Julius Mwaiselage, alisema taasisi hiyo itashiriki kikamilifu katika kambi hiyo hasa katika kupima na matibabu ya saratani.

Mwakilishi wa Taasisi ya Management Development for Health (MDH)  Isaack Laizer, alisema taasisi hiyo licha ya kusaidi kambi hizo kwa asilimia  70 utajikita kusaidia huduma za chanjo na upimaji wa Ukimwi.