MJAPANI WA GEITA ATEMWA


Na Mwandishi Wetu

Klabu ya Geita Gold imetangaza kuachana na wachezaji wake saba, akiwemo Shinobu Sakai raia wa Japan.

Shino alijiunga na Geita Gold mwaka jana na kubeba matumaini makubwa katika kikosi hicho, lakini ameshindwa kufikia matarajio ya klabu.

Geita Gold pia, imeachana na Fabrice Kayemba, Arakaza MacArthur, Shown Oduro, Mussa Gadi, Jeremiah Thomas na Daniel Lyanga ambaye tayari ametua JKT Tanzania.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Geita Gold, Simon Shija, amesema wanatarajiwa kuwaacha wachezaji 10.

Amesema hivi sasa wanaendelea na mazungumzo na wachezaji watatu wa kikosi hicho ili kuachana nao.

Shija amesema sababu ya kuachana na nyota hao ni kumaliza mikataba yao pamoja na wengine kutorodhika na viwango vyao.

“Mchezaji ambaye anamaliza mkataba na tupo katika mazungumzo nae ni Elias Maguri ambaye msimu uliopita alikuwa katika kiwango bora, wengine tutaendelea kuweka wazi tunapokuwa tunamalizana nao,” amesema.

Alisema wamepania kufanya vizuri msimu ujao, hivyo wanalazimika kujenga kikosi bora kitakachokuwa tishio.

Geita Gold msimu uliopiota ilimaliza Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa katika nafasi ya saba kwa pointi 37 b aada ya kucheza mechi 30.