CCM SINGIDA WATAKA WABUNGE NA MADIWANI WAELEZE WANANCHI FEDHA ZINAZOTOLEWA NA RAIS SAMIA KUTEKELEZA MIRADI YA MAENDELEO



Na HEMEDI MUNGA

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Martha Mlata, amewaagiza Wabunge na Madiwani wa mkoa huo kuwaeleza wananchi fedha nyingi zilizoletwa na  Rais Dk. Samia Suluhu Hassan,  katika maeneo yao kutatua kero mbalimbali kupitia miradi anuai.

Martha ametoa agizo hilo wakati wa kumkabidhi Mkandarasi atakayejenga barabara inayoanzia Kizaga wilayani Iramba hadi Sabasaba,  Singida Mjini.

"Ninatoa agizo kwa wabunge wote wa Singida hiki kinachofanyika hapa mkafanye katika majimbo yenu, fedha zilizokuja waiteni wananchi muwaeleze kuwa Rais Dk. Samia ameleta fedha kwenye majimbo na kata kutekeleza miradi mbalimbali," amesema.

Amemuomba  Waziri wa Ujenzi,  Innocent Bashungwa, kufikisha salamu kwa  Rais Dk. Samia  kuwa wananchi wa mkoa huo ni watulivu wanaendelea kuchapa kazi huku wakisubiri kumchagua kwa kishindo ifikapo 2025.

Aidha, Martha amewataka wananchi  kuendelea kumuamini Rais kwa sababu anakesha akiwaza namna bora ya kuendelea kuwatumikia wananchi na kutatua kila aina ya changamoto.

Kwa upande wa Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, amesema kuna haja ya kumshukuru Rais Dk. Samia kwa kuwa amekuwa mstari wa mbele kutekeleza  Ilani ya Chama.

Mwigulu amesema Rais Dk. Samia amewasaidia wananchi kukamilika kwa barabara hiyo watapeleka mazao yao kwa uhakika kutokana na mapinduzi katika miradi ya barabara.

"Tumshukuru Rais kwa utekelezaji wa Ilani bora  katika kila sekta," ameshukuru na kuongeza kuwa 

" Hayo yote tumpongeze Rais kwa kazi anayoifanya kwa sababu miradi ya aina hii inafanyika nchi nzima, hakika Mama Yupo Kazini,"

Naye  Mkuu wa mkoa huo, Peter Serukamba amemuhakikishia  Waziri huyo kuwa Rais Dk. Samia na CCM wapo salama katika mkoa huo.

"Tunashauku kubwa sana ya kumlipa Rais Dk. Samia, hilo tutaanza mwakani na kulimalizia 2025," amesema.

Amesema mkoa huo una  vijiji 441 takriban vyote vimepata nishati ya umeme huku ifikapo 2025 asilimia ya upatikanaji wa maji itafikia asilima 80.

Pia, kuhusu suala la mbolea amewataka wananchi hao kuhakikisha wanajiandaa kwa kuwa ifikapo tarehe 20 mwezi huu mbolea zitawafikia katika vijiji vyao.

Amefafanua kuwa barabara hii ya kilometa 77.6 kwa sh bilioni  88 inatekelezwa huku barabara ya kutoka Itigi kwenda  mkoa wa Mbea ikitengewa bilioni 60 na ile ya  kutoka Nduguti hadi Chemchem inakwenda kujengwa.

Katika kuhakikisha mkoa huo unakuwa chachu ya chakula, Serukamba amesema  anahitaji kuhakikisha Singida inaingia kwenye  ramani ya uzalishaji kwa kuwa inawatu wenye nguvu.

Pia, kulisha nchi hii kwa  mafuta ya kula huku vitunguu, dengu,  korosho, pamba, mpunga, mahindi na kuku vitoke Singida.

"Sisi tuna deni  na Rais Dk. Samia kwa kuwa anafanya mambo ambayo waliotangulia katika nafasi hiyo hawakuweza kufanya," amesema.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman  Mwenda, amemshukuru na kumopneza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuwakumbuka kuwaletea barabara ambayo itakuwa historia na ukombozi katika wilaya hiyo.

Mwenda amemuomba  Mkandarasi wa kampuni ya   Henan Highway engineering group kutoka nchini China, Huang LeLe  kutengeneza  barabara hiyo kwa viwango vinavyohitajika kutokana na thamani ya fedha.

"Mhe Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa sisi  wanairamba leo ni siku kubwa na yakipekee tena  ya kihistoria kwa wilaya yetu kwa kutimia barabara hii muhimu sana," amesema

Aidha, amesema kuwa kukamilika kwa barabara hiyo mbali ya kupata maendeleo  ya kiuchumi ispokuwa maafa yaliokuwa yakitokea  katika daraja la Usure hayatakuwepo.

Barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 77.6 na upana wa futi 10 inayojengwa kwa kiwango cha lami kwa sh bilioni 88 ikikamilika itaimarisha  uchumi wa wananchi wa wilaya hiyo.


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, akimuagiza Mkandarasi Huang LeLe atakayejenga barabara inayoanzia Kizaga wilayani Iramba mkoani Singida kuelekea Sabasaba Singida mjini kuhakikisha inakamilika kwa wakati, katika hafla ya uzinduzi wa ujenzi huo. (Picha Hemedi Munga).

Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, akizungumza na wananchi wakati wa hafla ya kukabidhi mradi wa ujenzi wa barabara inayoanzia Kizaga wilayani Iramba hadi Sabasaba Singida Mjini.


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa (kushoto), akimakabidhia Mkuu wa Wilaya ya Iramba, cheti kutambua kazi kubwa anayoifanya katika wilayani humo, wakati wa kumkabidhi mkandarasi atakayejenga barabara inayoanzia  Kizaga wilayani  hadi Sabasaba Singida mjini kwa kiwango cha lami. (Picha na Hemedi Munga).