DIWANI AMSHUKURU RAIS DK.SAMIA UTEKELEZAJI MIRADI YA MAENDELEO KATA YA KIGAMBONI

 

Diwani wa Kata ya Kigamboni, Dotto Msawa (kulia), akiwa na Kamati ya Siasa ya kata hiyo, wenyeviti wa serikali ya mtaa na wakikagua ujenzi wa barabara ya Chagani, wilayani Kigamboni.




Na Mwandishi Wetu

Diwani wa Kata ya Kigamboni, Dotto Msawa, amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwaletea fedha za ujenzi wa barabara, Shule ya Sekondari na ukarabati wa Soko la Feri.


Msawa ametoa shukrani hizo wakati akikagua ujenzi wa barabara ya Chagani, Shule ya Sekondari Paul Makonda na Soko la Feri, akiwa na kamati  ya Siasa ya Kata hiyo, wilayani Kigamboni.


Amesema wananchi wa kata hiyo wamefarijika kwa kuletewa fedha za miradi wa barabara Sh. milioni 894  ambazo zinajenga barabara ya kiwango cha lami katika  barabara ya Chagani hadi barabara ya Njama.


"Kwa niaba ya wananchi wenzangu tunamshukuru Rais Dk. Samia kupatiwa fedha  hizo katika kata yetu, zimesaidia katika ujenzi barabara ya Chagani yenye urefu wa kilometa 0.7, pamoja kuweka taa za barabarani 24,  vivuko vinne na mifereji ya maji mvua", amesema.


Msawa amesema mradi huo utakapokamilika utaondoa kero kwa wananachi wanaotumia barabara hiyo, ambayo awali ilikuwa mashimo na haikuwa na mifereji ya kupitisha maji ya mvua.


Akizungumzia kuhusu sekta ya elimu katika kata hiyo, Msawa amesema kuna ujenzi wa Shule ya ghorofa nne ya Sekondari Paul Makonda, unaendelea pamoja ujenzi wa maabara  mbili za kisasa kwa lengo wanafunzi kupata mazingira mazuri ya kupata elimu bora.


Amesema shule hiyo inawanafunzi wa kidato  cha kwanza hadi kidato cha nne,  baada ya kukamilika itakuwa na   uwezo wa kuchukua wanafunzi wa kidato cha tano na sita.


Msawa amesema bajeti ya shule hiyo ilikuwa zaidi ya  Sh. milioni 900 na hadi sasa zimetumika zaidi ya Sh. milioni 600 na ujenzi unaendelera vizuri.


Kwa upande wa soko la feri, Msawa amesema soko hi lo ni dogo lakini asilimia 90 ya wananchi wa Kigamboni wanapata huduma katika soko hilo, hivyo lazima likabaratiwe na kupunguza kero mbalimbali wafanyabiashara  na wananchi wanaotumia soko hilo.


Amesema changamoto katika soko hilo ni wakati wa mvua linajaa maji, wameamua kulikarabati kuondoa kero hiyo haraka kwasababu wamepata zaidi ya Sh. milioni 18 za ukarabati.


"Soko hili wakati wa mvua linajaa maji hivyo fedha hizi tulizopata tunaanza kutengeneza miundombinu ya maji ya mvua na majitaka, hii yote ni utekelezaji wa Ilani ya CCM", amesema.


Naye Mkuu wa shule hiyo, Moshi Malilo, amesema shule ilianza na jengo moja na hadi sasa tuna majengo makubwa matatu na ujenzi unaendelea ni jengo litakalokuwa na vyumba madarasa 16.


Malilo amesema wanampongeza Rais Dk. Samia kwa kuwekeza katika sekta elimu, hususan katika kata hiyo ambayo awali haikuwa na shule ya sekondari.


Tunampongeza Rais wetu Dk. Samia kwa kuwekeza katika elimu, tulikuwa na jengo moja lakini sasa tuna majengo 16 ya madarasa yanakwenda kukamilika na ujenzi wa maabara mbili za kisasa zinajengwa, pia tuwapongeza viongozi wa CCM wa kata hiyo pamoja na diwani kwa kuwa mstari mbele kufanikisha ujenzi huo", amesema.





".