MKUMBO AKOSHWA NA UWEKEZAJI SHULE YA BETHEL MISSION

 


Na Mwandishi Wetu

Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema anafurahishwa  mno na wawekezaji wanaojitokeza na kuwekeza katika ujenzi wa shule nchini na ameahidi serikali iko tayari kuwasaidia kwa hali  na mali wafikie malengo  waliojiwekea.

Hayo yameelezwa na Mkumbo ambaye ni Mbunge wa Ubungo, Dar es Salaam, wakati Maadhimisho ya miaka   25 ya Shule za Bethel Mission,  sambamba na Mahafali ya 19 ya wahitimu 32 wa darasa la saba wa shule hiyo iliyoko Makuburi.

Mkumbo amesema wadau na wawekezaji anapongeza kwa kufanya uwekezaji huo mkubwa katika sekta aya elimu, kwani alisema ni vigumu kwa kila kitu kikiachwa kifanywe na serikali pekee.

“Kikubwa hapa kwanza nawapongeza wamiliki wa shule hii ya Bethel Mission School, kwani uwekezaji huu ni mkubwa na umelenga kuiunga mkono serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kupunguza uhaba wa shule nchini,” alisema mbunge Mkumbo.

Amesema serikali  inawaahidi wamiliki wa shule hiyo na wengine, ambao wamewekeza  katika ujenzi wa shule kuendelea kufanya hivyo kwa kasi kubwa kwani serikali iko nyuma yao na inawaunga mkono.

  Naye,   Mkurugenzi wa shule hiyo, Emmanuel  Mshana, akizungumza katika maadhimisho hayo amesema shule yake ni miongoni mwa shule chache, ambazo zinaendeshwa na taasisi za kidini nchini lakini haina ubaguzi wa wanafunzi kwa kufuata dini zao.

Mshana amesema hatua hiyo kwa kina imesaidia wahitimu wanaomaliza katika shule hiyo, kuiva katika  taaluma, maadili na kumjua Mwenyezi Mungu. 

“Shule zetu hazimbagui mwanafunzi yeyote yule kwa dini yake, bali tunamwandikisha  mwanafunzi hata kama siyo wa  dini ya kikristo ila mwenye  sifa za kusoma kwetu,” amesema mkurugenzi Mshana.

Amesema katika shule hizo kuna somo la Biblia, lakini cha ajabu wanafunzi wanaofaulu vizuri somo hilo ni wale wanafunzi ambao siyo waumini wa dini ya kikristo.

 Mwenyekiti wa Kanisa la International Missionary Society SDA-Reform Movement, Mchungaji Hildon Mbogela alisema shule za Bethel Mission zitaendelea kuwa kimbilio kwa Watanzania wengi kutokana na ubora, maadili na kiwango cha elimu  wanachokitoa.

“Shule hizi zitaendelea kuwa kimbilio kubwa kwa wazazi wengi wa Kitanzania, kwani shule zetu ziko mstari wa mbele katika utoaji wa elimu bora na masuala mengine yamwezeshayo mtoto kumjua Mwenyezi Mungu ili wakaufikie mwisho mwema watakapoondoka hapa duniani,” alisema  mwenyekiti huyo.