RAIS DK. SAMIA AFUNGUA JENGO LA HOSPITALI YA RUFAA KANDA YA KUSINI MTWARA



Na Gregory Millanzi, Mtwara


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, leo September 15,2023 ametoa maagizo kwa wafanyakazi wa Hospitali ya Rufaa ya kanda ya Kusini kuhakikisha wanatunza vifaa na jengo na  wanatoa  huduma bora kwa wananchi kwa lugha nzuri. 

Rais Dk. Samia ametoa maagizo hayo wakati akifungua jengo la Hospitali hiyo ambapo amewataka wananchi wa Mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma kuitumia hospitali hiyo ili kuhakikisha wanapata huduma bora na kupunguza safari za kwenda Muhimbili kufuata huduma.

Pia Rais Dk. Samia amekabidhi magari matatu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini Kati yao mawili yakiwa ya wagonjwa (Ambulance)ambayo moja wapo lina huduma ya matibabu ya ICU  na moja kwa ajili ya ufuatiliaji.

Akikabidhi magari hayo Rais Dk. Samia, ameutaka uongozi wa hospitali hiyo kuhakikisha gari hizo zinatumika vizuri kwa makusudi yaliyokusudiwa.

"Hatutaki kuona gari limepakia magendo mnajidai Ambulance barabarani kumbe ndani  kuna mzigo haramu ,ikitokea hivyo dereva, aliyempa mali,na wewe msimamizi wote mnakwenda, gari zitumike kwa makusudi yaliyokusudiwa", amesema Rais Dk. Samia.

Rais Dk. Samia amesema jengo la hospitali hiyo halijajengwa kupamba mji, bali limewekwa kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi wote, pia kuhakikisha wananchi wanahudumiwa kwani kuna vifaa vingi na vya kisasa zaidi.

Aidha Dk. Samia ameutaka uongozi wa Hospitali hiyo kuhakikisha sauala la usafi linasimamiwa ipasavyo na ikiwezekana  itafutwe kampuni itakayo simamia usafi ili kuendelea kuwa bora .

Rais Dk. Samia yuko mkoani Mtwara kwa ziara ya siku nne kuanzia September 14  mapaka 17 ,2023  kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo leo September 15 ametembelea na kuzindua Hospitali ya Kanda ya Kusini, Bandari ya Mtwara, Chujio ya maji Mangamba, uwanja wa Ndege na uzinduzi wa barabara ya lami Mtwara hadi Mnivata.